KLABU ya Yanga imevuna kiasi cha Sh7 bilioni kwa mwaka kutokana na wadhamini mbalimbali wa timu hiyo.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa klabu hiyo, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said amesema kiasi hicho kimepatikana kwa msimu wa 2022/23 uliomalizika hivi karibuni.
"Tunawashukuru na kujivunia sana wadhamini wetu kwa sababu katika michezo mbalimbali tumetumia gharama nyingi hivyo tunajivunia uwepo wao," amesema
Aidha Hersi aliongeza mbali na fedha hizo zinazotoka kwa wadhamini kama SportPesa, Azam TV na Kampuni ya Haier inayojihusisha na usambazaji na utengenezaji wa vifaa mbalimbali vya ofisini na majumbani, ila Yanga imepata Sh3.5 bilioni kwa mwaka kutokana na ushiriki wao katika mashindano mbalimbali.
Yanga inafanya mkutano wake mkuu leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere (JNICC) ikiwa ni wa kwanza tangu uwaingize madarakani Rais wa klabu hiyo, Hersi Said, Makamu wa Rais, Arafat Haji na wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliochaguliwa Julai mwaka jana.