Mkuu huyo wa kundi la mamluki la Wagner Yevgeny Prigozhin, amevunja ukimya ikiwa ni siku mbili baada ya kuongoza uasi ulioshindwa akisema kwamba hakukusudia kuipindua serikali ya Moscow. Katika tamko lake la kwanza alilolitoa kwa umma tangu alipoonekana usiku wa Jumamosi akiviondoa vikosi vyake katika mji waliokuwa wameushikilia, Prigozhin ameongeza kuwa wapiganaji wake walisimamisha kampeni yao ili kuepusha umwagikaji damu.
"Tulienda kama ishara ya kupinga na sio kupindua serikali ya nchi", alisema mkuu huyo wa Wagner katika sauti ya dakika 11 iliyotolewa Jumatatu jioni kupitia mtandao wa Telegram. Prigozhin anadai azma yao ilikuwa ni kushinikiza masuala waliyoyaibua kipindi cha nyuma, hususan matatizo makubwa ya usalama wa nchi.Rais Putin wa Urusi aonekana kwa mara ya kwanza tangu uasi wa Wagner
Ndani ya sauti hiyo, Prigozhin anasikika akisema alitaka kuzuia uharibifu wa wapiganaji mamluki wa Wagner na kulazimisha makamanda waliohujumu kampeni ya kijeshi ya Urusi nchini ukraine kuchukuliwa hatua za kisheria. Prigozhin aliwatetea wapiganaji wake kwamba hawakuanzisha mapigano yoyote katika ardhi ya Urusi na kwamba anajutia kuidungua ndege ya kivita ya Moscow ambayo ilianza kuwashambulia.
Hata hivyo kiongozi huyo hajafahamisha juu ya wapi alipo au mipango yake ya baadae na hakutoa maelezo zaidi juu ya makubaliano yaliyo na utata yaliyosimamisha uasi huo. Siku ya Jumamosi Prigozhin alidai kwamba angeelekea nchi jirani ya Belarus chini ya makubaliano yaliyofikiwa na Rais Alexander Lukashenko.Urusi baada ya kitisho cha uasi
Wakati Prigozhin akitetea msimamo wake na kile alichokifanya, baadae kidogo Rais Vladimir Putin naye alitoa hotuba yake ya kwanza tangu kulipotokea uasi wa Jumamosi. Kwenye hotuba yake aliyoitoa kwa njia ya Televisheni, Putin amewashukuru Warusi kwa "uvumilivu, umoja na uzalendo", akiongeza kuwa "tangu mwanzo wa matukio" alitoa amri ya hatua kuchukuliwa ili kuepusha umwagikaji mkubwa wa damu." Aidha kiongozi huyo hakusita kuyashutumu kwa uwazi mataifa ya magharibi na Ukrainekwamba walitaka kuona Warusi "wakiuana wenyewe".
Nao, mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wamejadili juu ya uwezekano wa athari za uasi huo wa muda mfupi, walipokutana huko Luxemborg kujadili masuala ya usalama. Mwanadiplomasia mkuu wa Umoja huo Josep Borrell amesema hadi sasa "hali inabakia kuwa ngumu na isiyotabirika", huku waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baebock akiongeza kuwa mzozo wa kuwania madaraka nchini Urusi bado haujamalizika.
Vyanzo: Reuters/DPA/AP/AFP