Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameendelea kuibana Ofisi ya Taifa ya Mwendesha Mashitaka (DPP), baada ya kushauri uchunguzi ufanyike na ikibainika kulitokea ukiukwaji wa haki katika makubaliano ya kukiri makosa (plea bargaining), watuhumiwa warejeshewe fedha zao na kufutiwa rekodi za mashtaka.
Zitto alitoa ushauri huo jana mbele ya Tume ya haki jinai inayoendelea na kazi ya ukusanyaji maoni pamoja na uchambuzi kabla ya Juni 30, mwaka huu kukabidhi ripoti kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Tangu Sheria ya Makubaliano ya Kukiri Kosa (plea bargaining) ianze kutumika mwaka 2019, watuhumiwa wengi wa makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha waliokuwa mahabusu walitumia njia hiyo, ili kuwa huru.
“Nimeshauri watu wote walioonewa katika utaratibu ule ikibainika walipwe fedha zao, wafutiwe rekodi za makosa,” alisema Zitto. Wakati wa hafla ya kuwaapisha wajumbe wa tume hiyo mjini Dodoma, Rais Samia alisema malalamiko mengi yanaelekezwa katika ofisi ya DPP kuhusu wapi na kiasi gani cha fedha zilikusanywa chini ya utaratibu wa Plea Bargaining. Aidha, Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22 iliweka wazi kuwa aliyekuwa DPP na maofisa wake hawakusimamia mikataba hiyo huku wakikiuka taratibu za kukamata, kuendesha mashtaka na kushughulikia kesi za madai. Zitto alishauri pia kufumuliwa sheria za Jeshi la Polisi, ili kudhibiti malalamiko yanayohusu ukandamizaji wa raia ikiwamo mazingira ya ubambikaji wa kesi, kuanzisha kamisheni huru ya kusimamia madai yanayohusisha utendaji wa jeshi hilo na ukamilishaji wa upelelezi kabla ya kufungua kesi mahakamani. Pia alishauri kuimarishwa mfumo wa bajeti pamoja na uhuru wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). “Kianzishwe chombo maalumu ndani ya Takukuru kufuatilia na kudhibiti ufisadi na kuondolewa kwenye fungu la 20 la utegemezi wa bajeti ila wajitegemee wao,” alisema. Kabla ya Zitto, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (JWTZ), Jenerali Jacob Mkunda aliwasilisha maoni yake mbele ya tume hiyo jana asubuhi.