Mashabiki wa Yanga kwa sasa akili hazijatulia, hii ni kutokana na vuta nikuvute iliyopo baina ya klabu hiyo na straika Fiston Kalala Mayele.
Mwamba huyu aliyemaliza kama kinara wa mabao wa Yanga kwa misimu miwili mfululizo anataka kuondoka kikosini. Mabosi wa klabu hawataki kuona anaondoka kutokana na presha wanaoweza kuipata kutoka kwa mashabiki na wapenzi wa Yanga.
Mayele amefunga jumla ya mabao 33 katika misimu miwili ya kucheza Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi cha timu hiyo Alianza na mabao 16 msimu wa kwanza na kukikosa kidogo tu, kiatu cha dhahabu kilichoenda kwa George Mpole aliyekuwa Geita Gold aliyetupia mipira 17 nyavuni.
Kwa msimu huu amefunga 17 na kumaliza kama kinara akilingana na Saido Ntibazonkiza wa Simba, lakini akafunga mabao mengine 14 katika michuano ya CAF. Alifunga kwanza mabao saba katika mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kisha akafunga mengine saba katika Kombe la Shirikisho ambapo Yanga ilifika fainali na kuzidiwa na USM Alger ya Algeria iliytobeba kwa faidaya bao la ugenini, kwani matokeo ya jumla yalikuwa ni sare ya 2-2. Hapo hayajajumuishwa ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) wala Ngao ya Jamii.
PENGO LAKE
Yanga wanahofu kuondoka kwa Mayele wakitoka kufanya makubwa barani Afrika inaweza kuwapa ugumu wa kusaka mtu wa kurithi nafasi yake. Kumruhusu kuondoka ni kujitafutia majanga kutokana na ukweli ni wachezaji wachache wenye kariba ya Mayele.
Hata hivyo, Mayele ana maisha yake baada ya Yanga ndio maana anakomalia kuachiwa aondoke kutokana na ofa zenye donge nono zilizopo mezani mwa mabosi wa klabu hiyo na menejimenti yake.
Yote kwa yote ni lazima Mayele ataondoka tu Yanga, kwani hata kabla ya kuja kuichezea bado klabu ilikuwa na wachezaji wengine hata kama hawakufanya maajabu kama aliyoyafanya straika huyo kutoka DR Congo ambaye yupo kwenye kinyang'anyiro cha kusaka tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wanaocheza barani huyo inayoendeshwa na mtandao wa Foot Africa.
ANAJUA KUFUNGA
Mayele kama ilivyo kwa wachezaji wa nafasi yake ya ushambuliaji anajua sana kufunga na kutumia nafasi anazozipata.
Ni kweli kuna wakati nyota huyo alikuwa akipoteza nafasi za kufunga kwa kuwa na papara, lakini mara zote alikuwa akiwapa furaha mashabiki kwa kufanya maamuzi magumu kwa kupambana kwa jasho na damu ili kuamua matokeo ya pambano la timu yake, kitu kilichomjengea heshima.
Utabisha nini? Wakati kwenye mchezo wa nusu fainali kati ya Yanga na Marumo Galants ya Afrika Kusini alijipigia pasi kwa mbele kisha kuwatoka mabeki wa Sauzi na kufunga bao muhimu kwa Yanga lililoihakikisha kwenda fainali.
Pia alifanya maamuzi magumu nchini Nigeria wakati Yanga ikipambana na Rivers United na kupata ushindi wa mabao 2-0 ugenini, yotye akifunga yeye na kuiwezesha timu kusonga mbele kwenda nusu fainali licha ya kwamba mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam uliisha kwa suluhu.
Katika mechi ya fainali ya kwanza, Mayele alifunga bao muhimu lililokuwa la kusawazisha la Yanga dakika 82 na kuiweka pazuri Yanga kubeba taji kama sio uzembe uliosababisha USM Alger kupata bao la ushindi wa mabao 2-1 na penalti ya Djuma Shaban kule Algier ilifanya mechi kumalizika kwa 1-0. Kama sio Waalgeria kupata bao lile la pili, huenda Yanga ingetoka sare na kisha kwa matokeo ya ugenini ingewabeba.
Hii ni kuonyesha Yanga inapaswa kuwa na mchezaji wa aina gani ili kuziba nafasi ya Mayele. Ni kweli ina Kennedy Musonda, ina Stephane Aziz KI na wakali wengine wakiwamo waliosajiliwa kwa msimu ujao, ila bado kiwango cha Mayele kinawaacha mbali na hii ndio inaifanya Yanga isijiamini.
TUJIKUMBUSHE
Ulishawahi kuyasikia majina ya Abeid Mziba 'Tekero' na Makumbi Juma 'Homa ya Jiji' ama 'Bongabonga'? Kama huwajui basi, hawa majamaa walikuwa ni miongoni mwa mastraika mahiri waliowahi kutokea katika soka la Tanzania.
Asikuambie mtu, Tanzania ilibahatika kuwa washambuliaji hodari, waliokuwa hawafanyi makosa mbele ya lango la timu pinzani. Walikuwa wakitupia mipira kambani kama waliovurugwa akili. Victor Mkanwa, Said Mwamba 'Kizota', Mchunga Bakar 'Mandela', Said Mrisho 'Zico wa Kilosa', Mohammed Mateneke, Mohammed 'Bob' Chopa, Juma Mgunda, Duncan Butinini, Mohamed Hussein 'Mmachinga', Fumo Felician, Kitwana Seleman, Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio' na wengine walitisha.
Hao na wengine walikuwa ni kati ya hazina kubwa ya mastraika waliotisha enzi zao wakicheza. Miongoni mwao ndio hao kina Mziba na Makumbi, waliotamba na klabu mbalimbali zikiwamo RTC Kigoma na Yanga sambamba na timu ya taifa, Taifa Stars. Wawili hao waliokuwa hawashikiki kwa kufumania nyavu waliibuka na kutamba miaka ya 1980-90. Sifa kubwa ya Mziba ilikuwa ni umahiri wake wa kufunga kwa kichwa kama anayepiga kwa mguu. Sio kama hakuwa anafunga kwa mguu, la! Makumbi kwa upande wake, licha ya mbwembwe zile za wachezaji wanaotokea Kigoma enzi hizo, alikuwa pia ni fundi wa kufunga mabao kwa mashuti, kitu kilichofanya awe maarufu nchini. Kokote anakopita hadi sasa ni maarufu vilevile.
Sasa sikia mkasa wao. Inadaiwa wawili hao walikuwa wakipenda kutembea pamoja katika mitoko yao. Inaelezwa wakipita eneo kama la Mtaa wa Congo ambalo kwa miaka yote limekuwa na vurugu za kibiashara na kujaza watu. Mmoja anatangulia mbele na kujifanya kama amepoteana na mwingine, kisha kuitana majina. Inaelezwa hiyo ilikuwa mikogo yao ya kuwajulisha mashabiki wao kuwa walikuwa katika eneo hilo. Watu waliwapapatikia na kuwapa kila kilichowafaa kama ahsnate kwao.
Unajua miaka ya nyuma, wanasoka ndio waliokuwa wakipapatikiwa kuliko ambavyo leo kina Diamond, Harmonize, AliKiba na wenzake wanavyopapatikiwa mitaani na mashabiki. Walichokuwa wakikifanya kina Mziba na Makumbi ilikuwa mikogo tu ya kurahisisha maisha, lakini ni kule kujivunia umahiri wao wa kuwaburudisha mashabiki uwanjani. Kufunga mabao bwana raha sana na kunampa straika heshima kubwa!
ILIKUWA LAZIMA Ndio hawakuwa wao tu, wachezaji wengi nyota wa zamani walikuwa na mikogo yao na jeuri kwa vipaji vyao. Inadaiwa mikogo hiyo ilikuwa ikifanywa pia na kina Hamis Gaga 'Gagarino', ambaye alikuwa akitoka uwanjani anatinga kumbi za burudani jezi begani, kisha anazigida za bure za kutosha kisha kujirudia zake gheto kiroho safi.
Vivyo hivyo ilivyokuwa kwa 'Kizota' na wengine walioringia kazi kubwa waliyokuwa wakiifanya uwanjani. Inaelezwa kwamba mikongo na jeuri walikuwa nayo zaidi, washambuliaji. Hii ni kwa sababu walikuwa wakifunga kadri walivyopata nafasi na mabao yao yalizifanya timu zao kupata mafanikio. Walipapatikiwa na kila mashabiki, kuanzia wa kiume hadi wale wa kike.
Kwanini sasa wasiringe. Mabao lukuki ya vichwa aliyofunga Mziba, kwanini yasimpe jeuri? Mashuti aliyokuwa akiyafumua Joseph Machela, niliyemshuhudia mara ya mwisho jijini Arusha mwaka 1989 akiizamisha Simba kwa bao 1-0 wakati akiichezea Yanga katika michuano ya Kombe la AICC, iliyokuwa ikifanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha kwa nini yasimfanye asitembee kifua mbele? Ilikuwa lazima waringe. Wala hakuna aliyechukia kuona wakiringa. Kazi waliyokuwa wakiifanya uwanjani na kuzisaidia timu zao, ilikuwa ni hazina tosha.
HALI ILIVYO SASA Sasa ukipiga picha mbwembwe za wanaume hao wa zamani, rejea kwenye kizazi kilichopo sasa. Angalia wachezaji wanaocheza nafasi ya ushambuliaji na mbwembwe wanazozifanya. Waangalie wanavyotembea mitaani ama wanapoingia klabu kula bata. Fuatilia namna wanavyotamba kwenye kurasa za magazeti wakisema hili na lile la kujifagilia.
Wachungulie wanavyotupia picha katika akaunti zao za mitandao ya kijamii wakionyesha mbwembwe wanazofanya nje ya uwanja. Sijakuambia uangalia vichwani mwao walivyoa mitindo mbalimbali ama walivyozipaka rangi nywele zao. Yaani mabishoo sana, hata kama ubishoo wao hauwezi kuwafikia kina Hamza Maneno, Gaga, David Mjanja, Celestine 'Sikinde' Mbunga, Nsa Job na wengineo.
Cha kushangaza wanafanya mbwembwe na mikogo yote hiyo, wakati uwanjani ni weupe kabisa. Hawatishi kwa mabeki wala kuwatetemesha makipa kwa mabao. Yaani ni kama nyoka wa kibisa, wasiouma. Lakini wenyewe wanajitambulisha kuwa ni washambuliaji. Mshambuliaji gani anamaliza msimu hana hata bao moja? Straika gani anacheza mechi zaidi ya 25 akizidiwa mabao hadi mabeki au kiungo wa timu pinzani? Straika gani anayeweza kufungua kinywa chake kujitapa, wakati hata bao la off-side uwanjani katika msimu mzima hana. Straika asiyeitetemesha timu pinzani, ni vipi anaweza kwenda saluni kunyoa kiduku na kutengeneza madoido mengine kichwani mwake? Angalau Paul Pogba anaweza kuwa na jeuri ya kukaa nyuma ya kioo kutengeneza nywele zake, kwa kazi kubwa anayoifanya eneo lake la kiungo.
Cristiano Ronaldo anastahili kuwa bishoo kwa sababu rekodi za mabao zinambeba. Lionel Messi ana kila sababu ya kupaka blichi nywele na midevu yake kwa sababu, anaringia rekodi zake za mabao na mafanikio makubwa aliyoyapata katika soka. Inachekesha kuona straika ambaye msimu mzima kafunga mabao mawili ama matatu ya penalti akiendelea kujiita straika na roho yake ikaridhika kutembea kwa mikogo mitaani. Wanapata ujasiri huo kutoka wapi? Hawajisikii aibu mbele ya mashabiki wanaojua udhaifu wao?
Sawa ni kweli kwa zama hizi kumekuwa na ugonjwa ya kupatikana kwa mastraika wa enzi za kina Zamoyoni Mogella, Zubeir Magoha, Augustino Peter 'Tino' ama Innocent Haule, lakini bado mchezaji wa nafasi hiyo anapaswa kuumia asipoifungia timu yake. Jean Baleke, Mayele na hata Prince Dube unawaona wanavyoumia wanaposhindwa kufunga mabao, lakini hali hiyo huwezi kuona kwa washambuliaji wazawa. Huwezi kuona kwa Habib Kyombo wala Charles Ilanfya. Wao wakikosa wanatabasamu kana kwamba wamefanya jambo la kuvutia. Sura hazionyeshi kujutia. Hapa ni tatizo.
NINI KIFANYIKE
washambuliaji wa aina hiyo Kuendelea kuchukulia poa na kukomaa kujiremba kama wanamitindo na kutoa porojo zao magazetini eti wanataka kucheza soka la kulipwa nje ya nchi ni aibu kwao na kulifedhehesha taifa. Unatakaje kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya, wakati akiwa uso kwa uso na makipa kwenye Ligi Kuu ya Bara unatepweta, ndio utaweza kucheza mbele ya mabeki visiki vilivyopo Ulaya ambao wanachezea sifa na kutimiza wajibu wao kama wachezaji wa kulipwa?
Ni lazima vijana wanaocheza katika nafasi hizo na nyingine ndani ya timu zao, wabadilike na kujifunze kwa wachezaji wenzao waliowatangulia ndani ya nchi ama wale wanaokimbiza nje ya nchi. Hii itasaidia kujenga heshima yao na kama vile warejee tu ile mikogo ya kina Mziba ili wawakamue vilivyo mashabiki wao mitaani. Leo Yanga inahofia Mayele asiondoke kwa vile haina uhakika kama Crispin Ngushi ataweza kuibeba Yanga. Haiwezi kumuachia kirahisi Mayele wakati Yusuf Athuman amechemsha hata alipopelekwa Coastal Union kwa mkopo!
Lazima wachezaji wanaocheza eneo la ushambuliaji kuamka sasa na kujifunza kwa anachokifanya Meddie Kagere, Baleke, Mayele, Amissi Tambwe, Dube, Idris Mbombo na washambuliaji wengine wa kigeni ambao wamekuwa wa moto kiasi ya kuwatetemesha mabosi wa klabu wanazozichezea.
Lau kama hawa kina Ngushi, Clement Mzize wangekuwa wamekamilika kama Mayele, mabosi wa Yanga wasingekuwa na presha na hata mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo wasingeishia kwa mashaka ya kuhofia kuondoka kwa straika huyo Mkongoman. Ni kujipanga na kuamua tu. Kwao kwao!