Handeni. Watu saba wamejeruhiwa na mmoja kufariki dunia baada ya kugongwa na pikipiki ‘bodaboda’ usiku wa jana Jumapili, Julai 9, 2023 wilayani Handeni mkoani Tanga, wakati wakitoka mpirani.
Akisimulia mkasa huo, mmoja wa majeruhi, Amina Akida ambaye amelazwa hospitali ya mji Handeni, leo Jumatatu Julai 10, 2023 amesema, walikuwa wakitoka kwenye mpira ghafla ilitokea pikipiki ikiwa haina taa na kuwagonga.
Amesema pikipiki hiyo ilikuwa kwenye mwendokasi na ilipofika sehemu waliopo waliona taa zimezima na kuwagonga ambapo wameumia maeneo tofauti.
Mkuu wa wilaya ya Handeni, Albert Msando amesema ajali hiyo ilitokea usiku ambapo mtoto wa miaka 14 amepoteza maisha huku wengine saba wakijeruhiwa na wanaendelea na matibabu Hospitali ya Mji Handeni.
Amesema mhusika aliyesababisha ajali hiyo ni askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Handeni na tayari anashikiliwa na jeshi la polisi kwaajili ya hatua zaidi ya kisheria.
Mganga Mkuu halmashauri ya Mji Handeni, Dk Feisal Said amesema katika majeruhi hao saba wawili wamesafirishwa kwenda hospitali ya rufaa Bombo huku waliobaki wakiendelea na matibabu.