ATCL yalia na mzigo wa gharama za uendeshaji

ATCL yalia na mzigo wa gharama za uendeshaji


Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limesema linaendelea kupambana katika ushindani wa soko la usafiri wa anga, licha ya kukabiliwa na mzigo wa hasara unaoendelea kupungua.


ATCL pia inakabiliana na changamoto ya gharama za ukodishaji wa ndege kutoka kwa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), unaoathiri sehemu kubwa ya gharama za uendeshaji.


Kwa sasa ATCL ina ndege 12; moja aina ya Dash 8-Q300, tano aina ya Dash 8-Q400, nne aina ya Airbus A220-300 na mbili aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na ya 13 ya mizigo pekee iliyoingia hivi karibuni.


Hata hivyo, ATCL imesema kwa mwaka mmoja sasa imekuwa ikitumia ndege moja tu aina ya Airbus A220-300 yenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 120 hadi 160.


Katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Jumatatu hii, Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema pamoja na juhudi za Serikali kuongeza ufanisi wa shirika hilo, utaratibu wa ukodishaji wa ndege umeendelea kuwarudisha nyuma kutokana na gharama kubwa za uendeshaji.


Alipoulizwa swali kuhusu mwenendo wa shirika hilo katika kuzalisha mapato, Matindi alisema unaridhisha kwa kuakisi malengo ya kila mwaka ya shirika hilo, hususan katika kupunguza hasara: “Bado gharama zetu za uendeshaji ni kubwa sana kwa sababu ndege tunakodi. “Ingawa Serikali imeendelea kulifanyia kazi suala hilo, inaangalia namna gani shirika linaweza kujiendesha kwa tija zaidi, kupunguza mizigo inayowezekana,” alisema, akifafanua namna wanavyopambana wakati Serikali ikionyesha utayari wa kusaidia kuongeza tija.


Alisema katika kipindi cha ugonjwa wa Uviko-19, mwaka 2020/21 shirika hilo lilikabiliwa na changamoto zaidi, ikiwamo kutopunguza hasara, badala yake kuongeza.


Alisema baadhi ya mashirika makubwa duniani yalipewa ruzuku na Serikali zao, lakini wao hawakupewa.


“Tulisimamisha safari zote za nje, tukapunguza za ndani. Mashirika mengi hadi Marekani yalipewa ruzuku ili kuyanusuru. Lakini sisi hatukupata. Wala hatukupunguza mfanyakazi hata mmoja, ila tulipunguziana tu baadhi ya matumizi na posho za kawaida,” alisema.


Alisema kipindi hicho ndio ilikuwa mtihani mkubwa katika utendaji wake wa kazi kwa kushirikiana na watumishi wenzake wa shirika hilo, hivyo alitumia mbinu ya kuongeza safari za mizigo nje ya nchi na kuvuka hatua hiyo ulikuwa ni ushindi.


Kuhusu safari za mizigo, Matindi alisema bado kumekuwa na changamoto inayoendelea kuathiri bidhaa za Tanzania kukosa utambulisho wa kimataifa, huku mahitaji ya usafirishaji wa mizigo nchini yakiwa makubwa kuliko uwezo wa shirika.


Fidia ya ndege


Katika hatua nyingine, Matindi alisema kampuni iliyotengeneza injini mbili za Airbus A220-300 zinazofanyiwa matengenezo, imeanza kulipa fidia kwa Serikali kutokana na hasara ya kutotumika tangu Oktoba mwaka jana, ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kimkataba.


Hatua hiyo inakuja baada ya kampuni hiyo kushindwa kuwa na injini za ziada na hivyo kuwasababishia hasara wateja wake, ikiwamo Tanzania.


Kwa mujibu wa ATCL, kati ya ndege hizo 12, tatu hazifanyi kazi kwa sababu za kiufundi, zikiwemo hizo Airbus mbili.


Katika ufafanuzi, Matindi alisema kampuni hiyo pekee itaendelea kulipia fidia kwa maelekezo ya kimkataba hadi ndege zote zitakapokamilika Septemba mwaka huu, na kuanza kufanya kazi chini ya ushirikiano wa Shirikisho la Mashirika ya Ndege Afrika (AFRAA).


Alisema kusimama kwa ndege hizo kumesababisha athari ya utoshelevu wa mahitaji katika safari za masafa ya kati. “Kuna mkataba wa kununua injini na mkataba wa kununua ndege, kwenye mkataba huo wa injini kuna kipengele husika cha fidia. “Ndege hizo zitakuwa tayari hadi mwishoni mwa Septemba mwaka huu, fidia yake inatokana na mazingira ya soko. Lakini pia tunaweza kuzipeleka mashariki ya kati kwa Dubai, Oman,” alisema.


Juhudi, matumaini


Matindi alisema kwa sasa wastani wa ujazo wa abiria umeongezeka kutoka asilimia 53 mwaka 2015 hadi asilimia 80 mwaka jana, huku ikiendelea kutafuta fursa ya safari mpya za abiria na mizigo ndani na nje ya nchi.


Alifafanua kuwa mwaka 2016, alikuta shirika hilo likiwa na hasara karibu Sh110 bilioni, lakini imeshuka hadi Sh33 bilioni mwaka jana. Pia, shirika hilo halikuwa na kumbukumbu ya ripoti za fedha, lakini kwa miaka mitano mfululizo ATCL ina hati safi za ukaguzi kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).


Alisema kwa miaka minne mfululizo, ATCL limepewa ithibati ya huduma kwa viwango vya kimataifa chini ya Shirika la Kimataifa la huduma za usafiri wa anga (IATA), huku ikijenga mahusiano ya kibiashara na kampuni kubwa 10 za usafiri wa anga duniani, zikiwamo Qatar, Emirates, KQ na Ethiopia.


Pia, Julai mwaka jana, ATCL ilichaguliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la masuala ya usafiri wa Anga na Teknolojia (SITA Aero), likiwa pekee Afrika kati ya wajumbe 14 duniani.


Matindi alisema mahitaji makubwa ya ndani kwa sasa ni mikoa ya Mwanza, Kigoma, Kilimanjaro, Mbeya na maeneo chipukizi ya Songea, huku wakijipanga kurejea Mtwara.


“Tunategemea kati ya Agosti hadi Desemba kupokea ndege nyingine mbili za masafa ya kati Boeing 737 MAX 9, zenye uwezo wa kubeba abiria 180,” alisema.


Matindi alisema ndege hizo zitaongeza vituo vipya vya Sudan Kusini, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.


Kwa sasa shirika hilo linahudumia safari za ndani, kikanda na kimataifa kupitia safari zake takribani 120 kwa wiki katika vituo 15, vikiwamo 10 vya hapa nchini. Kwa mujibu wa shirika hilo, kabla ya kufunga mwaka huu, linatarajia kuongezewa ndege nyingine moja aina ya Dash 8 Q400, moja aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na moja aina ya Boeing 767 Freighter.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad