Shinyanga. Mzee Amos Samson (65), mkazi wa Kijiji cha Mwamala Wilaya ya Shinyanga, anatuhumiwa kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 16 (jina linahifadhiwa) baada ya kumrubuni kwa kumpa Sh7, 000.
Mwanafunzi huyo wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kolandoto Manispaa ya Shinyanga alikubali kujihisisha kimapenzi na mzee huyo baada ya ushawishi wa awali wa Sh2, 000 kabla ya baadaye kuongezewa Sh5, 000.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi ameiambia Mwananchi kuwa suala hilo tayari limeripotiwa na kwamba Jeshi la Polisi linamsaka mtuhumiwa aliyefanikiwa kutoroka baada ya taarifa hizo kufichuka.
Kwa mujibu wa Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dk Luzila John, vipimo vya kitabibu vimebainisha kuwa mwanafunzi huyo ana ujauzito wa miezi mitano.
Alivyorubuniwa
Akizungumza na Mwananchi mwanafunzi huyo amesema katika tukio la kwanza, mtuhumiwa alimshawishi kwa kumpatia Sh2, 000 ndipo akakubali kukutana naye kimwili.
Anasema katika tukio la pili, mtuhumiwa mara ya kwanza mzee alimwita nyumbani kwake na baada ya kumwingilia kimwili alimpatia Sh5, 000.
Amesema taarifa za uhusiano wao wa kimapenzi uliodumu tangu Desemba, 2022 zilibainika baada ya mzee huyo kumtaka kimapenzi ndugu yake mwingine wa kike ambaye aliamua kufichua jambo hilo kutokana na kuchukizwa na tabia ya mtuhumiwa ya kutaka kuwa na uhusiano nao wote wawili.
Baada ya taarifa hizo kufikia familia, juhudi za kijamii za kulimaliza suala hilo kwa mtuhumiwa kupigwa faini ya gunia mbili za mpunga na baiskeli zilifanyika.
Katika jitihada hizo, mtuhumiwa aliyekuwa miongoni mwa viongozi kijijini hapo aliondolewa kwenye nafasi ya uongozi, hali iliyoibua udadisi kutoka kwa wananchi, ndipo ikabainika kuwa anatuhumiwa kwa ukosefu wa maadili kutokana na kudaiwa kumpa ujauzito mwanafunzi.
"Ufuatiliaji wa wananchi ndio uliowezesha tabia chafu ya mtuhumiwa ya kuwaribuni watoto kimapenzi ikiwemo kumpa ujauzito mwanafunzi kujulikana," amesema mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Mwamala kwa sharti la kuhifadhiwa jina
Katibu wa kampeni ya kupinga ukatili (SMAUJATA) Mkoa wa Shinyanga, Daniel Kapaya, ameviomba vyombo vya dola na mamlaka nyingine husika kuhakikisha mtuhumiwa anapatikana na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
"Hatua za kisheria lazima zichukuliwe dhidi ya wote wanaofanya vitendo vya aina hii ili kuwa fundisho kwa wengine," ameshauri Kapaya