MUDA mfupi baada ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangaza kumfuta uanachama mtoto wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Balozi mstaafu Ali Abeid Karume, kupitia kikao cha usiku wa manane, mwenyewe aibuka na kusema atakata rufani kupinga uamuzi huo.
Balozi mstaafu Ali Abeid Karume.
Akitangaza uamuzi huo uliotokana na maazimio ya kikao cha Halmaushauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kusini Unguja kilichofanyika saa saba usiku, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM mkoa huo, Ali Timamu Haji, alisema kuwa mbali na uamuzi huo, pia wanamtaka Balozi Ali arejeshe kadi waliyompatia.
Ni uamuzi uliofanyika muda mfupi baada ya kada huyo kuzungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake na kukishutumu chama chake kuwa na utaratibu anaopingana nao - watu wasio na uzoefu kupewa nafasi za uongozi serikalini.
Haji alisema uamuzi huo umetokana na mwenendo wa kada wao huyo kukiuka maelekezo ya maadili, miongozo na nidhamu.
Juzi, kada huyo, mbele ya waandishi wa habari, alikishauri chama hicho kuepuka kufanya alichokiita makosa ya uteuzi kwa wanachama wake ambao hawajawahi kushika nafasi za chini za kisiasa na kiserikali kupewa nyadhifa za juu.
Alionya kwamba uteuzi wa aina hiyo unasababisha chama hicho kupata viongozi aliowaita dhaifu, wasiojua maana ya siasa, uongozi na utawala.
Mwandishi alipomtafuta Balozi Ali jana kuzungumzia uamuzi wa kufukuzwa CCM, alisema ameona taarifa hiyo katika mitandao ya kijamii, kwamba CCM Mkoa wa Kusini Unguja kupitia Kamati ya Halmashauri Kuu ya CCM, imemfukuza uanachama. Hajapokea barua yoyote.
Balozi Ali alisema hana mpango wa kurejesha kadi ya CCM wala kwenda chama kingine cha siasa.
Alisema kwa sasa anasubiri barua hiyo na atakapoipata, atakata rufani ya kupinga uamuzi katika Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ya CCM kwa sababu ni haki yake ya kikatiba.
“Nimesikia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii uamuzi uliochukuliwa, sijaitwa, wala kupewa nafasi ya kujieleza. Lakini kama uamuzi umeshapita, ninasubiri barua rasmi ili nikate rufani kwa sababu nina haki yangu," alisema.
Balozi Ali alisema ana wasiwasi juu ya uhalali wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa kilichotoa uamuzi wa kumfukuza uanachama wake.
UAMUZI WA CHAMA
Akitangaza uamuzi huo, Haji alisema umefikiwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022.
Alisema uamuzi huo ni kwa mujibu wa Ibara ya 89 inayoeleza kazi za Halmashauri Kuu ya Mkoa inayoelekeza kuangalia mienendo ya wanachama na viongozi wa CCM wa ngazi ya mkoa kichama na kulazimika kutoa taarifa kwa vikao vinavyohusika ngazi za juu.
Pia, alinukuu Ibara ndogo ya 14 kifungu kidogo cha 14, ambacho kinaelekeza kumwachisha au kumfukuza uanachama mwanachama yeyote endapo itadhihirika kwamba tabia na mwenendo wake vinamwondolea sifa za uanachama wake.
Kadhalika, alisema kifungu hicho kinasema mwanachama anayeachishwa au kufukuzwa uanachama anaweza kukata rufani kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
Timamu alisema kutokana na kupewa nguvu na Katiba ya CCM, waliotoa uamuzi walijiridhisha kwa kina kuhusu madai ya kukiuka maelekezo ya kikatiba na kupitia mapendekezo yote yaliyopokewa kutoka ngazi za tawi, wadi, jimbo na wilaya ambazo ni ngazi za chini za mkoa huo.
Alisema Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa huo imeridhia na kuridhika kwamba kutokana na kauli na vitendo vya mwanachama huyo, wamekubaliana kumwachisha uanachama wa CCM na kumtaka arudishe kadi ya uanachama ya kielektroniki namba C000/2809/993/1 ya Machi 17 mwaka 2022.
“Mwanachama huyu ameitwa na kuonywa kwa maandishi na vikao mbalimbali vya CCM, lakini hakutii wala kubadilisha tabia na vitendo vyake na kuendelea kukiuka kwa makusudi maadili na miongozo ya CCM.
“Hivyo, kwa mamlaka tuliyopewa na Katiba yetu ngazi ya Mkoa ya CCM Kusini Unguja, kwa kauli moja tumefikia uamuzi na makubaliano ya kumwachisha na kumfukuza uanachama mwanachama huyu," alisema.
WASIFU WAKE
Balozi Ali amewahi kushika nafasi mbalimbali za chama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zikiwamo kuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya, Mkoa, Mwakilishi wa kuteuliwa, Waziri wa Mawasiliano, Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Waziri wa Vijana na Michezo Zanzibar na Balozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali.
Balozi Ali alizaliwa Mei 24, 1950. Ni mtoto wa kwanza wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume, pia ni ndugu wa Rais mstaafu wa Awamu ya Sita Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Mwaka 2005 na 2010 alijitosa kugombea uteuzi wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kupeperusha bendera ya CCM, lakini hakuteuliwa.
Akiwa na miaka 28, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri, Wizara ya Biashara na Viwanda katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kazi aliyoishikilia kwa miaka sita (1972 – 1978) alipoomba likizo na kwenda kujiendeleza zaidi kimasomo Marekani.
Balozi Ali alianza kufanya kazi za kibalozi mwaka 1989 alipokuwa Balozi wa Tanzania na Marekani.
Mwaka 1993 alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Masuala ya Ulaya na Marekani katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania hadi mwaka 1996 alipopelekwa Ubelgiji kuwa Balozi wa Tanzania kwa nchi za Ubelgiji, Uholanzi, Luxembourg na Umoja wa Ulaya.
Mwaka 2002 alikuwa Balozi wa Tanzania katika nchi za Ujerumani, Uswizi na Poland sambamba na kuangalia uhusiano na nchi za Australia, Jamhuri ya Czech, Slovakia, Hungary, Romania na Bulgaria.
Kuanzia mwaka 2006, aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Balozi wa Tanzania katika nchi za Italia, Ugiriki, Uturuki na Malta. Pia amekuwa Balozi wa Tanzania Cyprus na Mkuu wa Mabalozi wa Tanzania.
*Imeandaliwa na Rahma Suleiman na Is-Haka Omar