Bei ya Sukari Yapaa, Vilio Sasa Maeneo Mengi nchini

 


Kupanda kwa bei ya sukari kumeanza kutikisa nchini, licha ya sababu za ongezeko hilo kutotajwa moja kwa moja.


Mwananchi limefanya uchunguzi sokoni na kubaini kuwa hadi jana baadhi ya maeneo bei imeongezeka hadi kufikia Sh4,000 kwa kilo moja.


Katika miji ya Musoma na Bukoba, bei ya sukari imepanda kutoka Sh2,800 hadi Sh3,300 na maeneo mengine ya Kanda ya ziwa bei ikibaki Sh2,800 hadi Sh3,000.


Mfanyabiashara wa nafaka na vyakula mjini Bukoba, Rahima Abdul alisema kilo moja ya sukarai inauzwa kati ya Sh3,000 hadi Sh3,300 na bei hiyo imeanza Juni mwaka huu. Kabla ya hapo kilo moja ilikuwa ikiuzwa Sh2,700.


“Mwishoni mwa Mei, 2023 wakati sukari inapanda, wafanyabishara wa maduka ya jumla walidai kuwa wakala aliyekuwa akiwasambazia, aliwauzia kwa bei ya juu kwa kuwa hata kiwandani bei ilipanda kutokana na upungufu,” alisema Abdul.


Bei ya sukari mjini Musoma imepanda kutoka Sh2,800 kwa kilo moja hadi Sh3,000 na 3,200 kwa kipimo hicho.


Mikoa ya Mwanza, Tabora, Kigoma, Simiyu, Shinyanga na Geita bei ya sukari ipo vilevile tangu mwaka jana ambapo kilo moja ni kati ya Sh2,800 hadi Sh3,000.


Mkoani Arusha kuna uhaba wa bidhaa hiyo muhimu katika baadhi ya maeneo na bei imepanda hadi kufikia Sh4,000 kwa kilo moja kutoka Sh2,800 katika maduka, husuan maeneo ya wilaya za pembezoni, zikiwamo Ngorongoro na Longido.


Mfanyabiashara Paul Dudui wa eneo la Wasso Loliondo, alisema sukari imeadimika katika mji huo na kusababisha adha kubwa. "Hapa Loliondo kuna maduka yanauza Sh3,600, wengine Sh3,800, vijijini huko imefika Sh4,000 kwa kilo," alisema.


Muuzaji wa jumla katika eneo la Sakina jijini Arusha, William Swai alisema bei ya jumla kwa kilo 50 imepanda kutoka Sh125,000 hadi Sh134,000 na bado inapanda.


Swai alisema taarifa kutoka kwa mawakala wakubwa ni kuwa bei imepanda kutokana na kusimama uzalishaji katika kiwanda cha TPC Moshi ili kupisha ukarabati.


"Sukari ambayo inatoka Mtibwa na Kilombero ni kidogo, pia kuna sukari inatoka Babati ambayo pia ni kidogo," alisema.


Rehema Lukumay, ambaye ni mfanyabiashara wa chakula katika eneo la soko kuu, aliomba Serikali kuingilia kati, kwani kila kipindi kama hiki bei imekuwa ikipanda kwa sababu mbalimbali na zikibadilika hazishuki.


"Chai tunauza kikombe Sh500 ila kwa hii bei ya sukari tunalazimika kupandisha hadi Sh700, lakini wateja wanalalamikia," alisema.


Kwa upande wa Mkoa wa Kilimanjaro, sukari imepanda kutoka Sh122,000 hadi Sh 130,000 kwa mfuko kwa kilo 50. Wafanyabiashara wa mjini Moshi waliliambia gazeti hili kuwa sukari imepanda bei kuanzia Juni, 2023 na hakuna sababu zilizoelezwa.


Venus Cistantine, alisema kutokana na bei kupanda katika naduka ya jumla, wanalazimika kuuza kilo moja Sh3,000 huku baadhi ya wafanyabiashara wakikwepa kuuza bidhaa hiyo.


Alisema kupanda kwa bei ya sukari kumewafanya baadhi ya wafanyabiashara kushindwa kuinunua baada ya kumaliza mzigo wa nyuma.


Mkazi wa mtaa wa Nyunguu mjini Babati, John Tluway alisema wafanyabiashara wa maduka ya rejareja waliongeza bei ya sukari hadi kufikia Sh3,500 hadi Sh4,000 kwa kilo moja kutoka Sh2,800.


"Hapa Babati kuna viwanda kadhaa vya sukari, ila kuna kimoja kinachosababisha sukari kupanda sijui ni nini ilhali tunalima miwa mingi hapa kwetu," alisema Tluway.


Mbunge mstaafu wa jimbo la Babati Vijijini, Vrajlal Jituson alisema ni kawaida katikati ya mwaka bei ya sukari kupanda kutokana na kutokuwepo kwa uzalishaji wa sukari, lakini kuna matumaini kuwa hivi karibuni bei itarudi kuwa kawaida.


Mkoani Morogoro bei ya sukari kwenye maduka ya rejareja imeendelea kuwa ni Sh2,800 kwa kilo moja licha ya bei ya jumla kupanda kutoka Sh61,000 kwa mfuko wa kilo 25 hadi kufikia Sh66,000.


Akizungumza na Mwananchi, mmoja na wafanyabiashara wa sukari, Devota Minja alisema bei hiyo imepanda mapema wiki hii na mabadiliko hayo yameanzia viwandani.


"Kwa uzoefu wangu kwenye biashara hii ya sukari, kila ifikapo miezi hii bei ya sukari imekuwa ikipanda," alisema Devota.


Wasemacho wazalishaji


Msemaji wa kiwanda cha Azam Group, Hussein Sufiani, alisema kiwanda chao kilifungwa tangu Novemba 2022 na wamefungua Julai 10 mwaka huu.


Alisema wana utaratibu wa kufunga viwanda kipindi cha masika ambacho huanza Aprili hadi Juni, kwani uvunaji wa miwa huwa mgumu.


"Inawezekana upungufu wa sukari umetokea kutokana na hali ya hewa na upatikanaji wa sukari ukawa umeyumba, lakini naamini na wenzetu watakuwa wameanza uzalishaji," alisema Sufian.


Naye Ofisa mtendaji wa kampuni ya TPC Limited inayomiliki kiwanda cha sukari cha TPC, Jaffary Ally, alisema jana kuwa tayari wameanza uzalishaji katika msimu mpya wa kuanzia Juni 22, 2023 ambapo tani 5,800 tayari zimeingizwa sokoni.


"Sukari iliyozalishwa msimu uliopita tulimaliza kuuza na kuingiza kwenye soko Juni 15 (2023) na Juni 22 tukaanza uzalishaji na tumeingiza sokoni tani 5,800 tayari. Kwa hiyo hatutegemei kuwe na upungufu wa sukari, labda kuwe na sababu nyingine," alisema Ally, alipohojiwa na gazeti hili


Meneja uendeshaji wa kampuni ya Superdoll Group ambayo inamiliki viwanda mbalimbali, vikiwemo vya sukari vya Mtibwa na Kagera, Abel Magese aliliambia gazeti hili kuwa viwanda vyao havijapandisha bei, pengine kilichotokea kinatokana na gharama za usafiri.


“Labda bei imepanda sababu ya gharama za usafiri wa eneo husika. Kwa miaka minne iliyopita haijawahi kutoka katika bei yake halisi licha ya kuwa kuna mazao mengi yamepanda bei," alisema Magese.


Katibu Mtendaji wa Chama cha Wazalisha sukari nchini, Deo Lyatto naye alimuunga mkono Magese akisema mara nyingi hakuna bei maalumu kutokana na usafirishaji wa maeneo inapopelekwa sukari, lakini kwa upande wa wazalishaji hakuna mabadiliko ya bei viwandani.


"Wakati viwanda vikiwa vimesitisha uzalishaji hakukuwa na upungufu wa sukari wala malalamiko ya upandaji wa bei, hivyo inashangaza kusikia baada ya kufunguliwa kwa viwanda bei imepanda," alisema Lyatto huku akihoji hilo linawezekanaje.


Mwananchi lilifanya juhudi za kuwapata viongozi wa Serikali kuzungumzia kinacholalamikiwa mtaanii bila mafanikio.


Alipotafutwa Waziri wa Viwanda na Biashara simu yake haikupatikana na Naibu wake, Exaud Kigahe alisema hataweza kusema lolote hadi Waziri wake atakapozungumza.


Kwa upande wa Wizara ya Kilimo, Waziri Hussein Bashe na Naibu wake Anthony Mavunde, walipotafutwa simu zao ziliita bila kupokelewa.


Hali ya uzalishaji na mipango ya Serikali


Uzalishaji wa sukari msimu wa mwaka 2022/2023 ulikuwa tani 456,019.73 ambayo ni sawa na asilimia 101.3 ya malengo ya uzalishaji yaliyokuwa yamewekwa na Serikali ya kuzalisha tani 450,000.


Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, nakisi ya sukari nchini ni tani 30,000, lakini kuna ongezeko la viwanda vipya vya sukari, vikiwemo viwanda vya Bagamoyo na Mkulazi.


“Kiwanda cha Sukari Bagamoyo kimeanza uzalishaji Agosti, 2022 ambapo hadi kufikia Aprili 2023 tani 18,127.2 za sukari zimezalishwa. Kadhalika, Kampuni ya Mkulazi Holding Limited inaendelea na usimikaji wa mitambo yenye uwezo wa kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka ambapo usimikaji umefikia asilimia 73.


“Hii itasaidia kupunguza nakisi ya sukari kutoka nje kwa kiwango kilichopo sasa cha tani 30,000 ili kufikia mwaka 2025 kusiwepo uagizaji wa sukari kutoka nje ambapo uzalishaji wa miwa unatarajiwa kufikia tani 7,000,000 ambazo zitazalisha tani 700,000 za sukari,” alisema Wazili wa Kilimo, Hussein Bashe wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake bungeni Mei mwaka huu.


Alisema Wizara imepanga kuanza kilimo cha umwagiliaji katika zao la miwa kwa wakulima wadogo wa Kilombero na ili kupunguza gharama za uingizaji wa sukari, Serikali itafanya majadiliano na viwanda vyote namna ya kuzalisha sukari ya viwandani, na kutumia mfumo wa sukari ya matumizi ya kawaida ili kulinda viwanda vya ndani.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad