Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei ya kikomo cha bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini ambapo bei ya petroli imeshuka katika baadhi ya mikoa.
Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia Jumatano, Julai 5, 2023, saa 6:01 usiku. Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo na kusainiwa na Mkurugenzi wa Ewura, Dk James Mwainyekule ilisema bei za rejareja za mafuta ya petroli na dizeli yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimeshuka kwa Sh 137 kwa lita na Sh 118/lita, mtawalia ikilinganishwa na bei za toleo la Juni 7 mwaka huu.
Pia, bei ya rejareja ya mafuta ya taa kwa Julai mwaka huu, itaendelea kuwa ni ile iliyotangazwa katika toleo la Juni 7, mwaka huu kwa kuwa hakuna shehena iliyopokelewa mwezi Juni mwaka huu.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara), bei ya rejareja ya mafuta ya petroli imeshuka kwa Sh 188 kwa lita wakati bei ya mafuta ya dizeli imeongezeka kwa Sh 58 kwa lita ikilinganishwa na bei za toleo la Juni 7, mwaka huu