Biashara, maisha Chato katika wakati mgumu



 “Mara ya mwisho kushuhudia wageni wengi na kupata hela nyingi ni wakati wa msiba wa Rais Magufuli”

“Tangu wakati huo biashara haijawahi kurudi katika viwango vilivyokuwepo. Hapa Chato nyumba za kulaza wegeni nyingi zilijengwa kuanzia mwaka 2016 sasa hazijazi tena kama zamani,” anasema Joseph Gadius ambaye ni mfanyabiashara wa nyumba za kulaza wageni.

Gadius anasema enzi za Rais Magufuli akiwa Chato kwa mapumziko au kwa sababu nyingine yoyote, wageni walikuwa wengi katika mji huo lakini  walikatika baada ya kifo chake.

“Hapa katikati biashara ilikuwa mbaya na wengine fedha walizotumia kuwekeza wamekopa kwenye taasisi za fedha, lakini kuna ahueni mpya baada ya hii hospitali ya rufaa kuanza kufanya kazi, wageni kidogo wameongezeka, hivyo baadhi ya ‘lodge’ zinapata wateja na nyingine zimegeuzwa vyumba vya kupangisha kwa wafanyakazi wa hospitali,” alisema Gadius.


“Unaona hiki chumba ulicholala ninapangisha Sh30,000 kuna wakati kilikuwa Sh50,000 kwa siku na watu wanagombania, sasa hivi wageni wachache labda kukiwa na taasisi fulani inafanyia semina, kidogo inakuwa afadhali,” alisema.

Chato ile si ya sasa

Kama haujatembelea Chato hivi karibuni, mji huo ukiuangalia  kutokea mbali na hata baada ya kufika katikati utapata picha ya mji unaokua kwa sababu ya majengo mengi mapya kama ilivyo kwa miundombinu mingine kama vile barabara na mingine inayoendelea kujengwa.

Chato ni mji uliopangwa vizuri na karibu barabara katika mitaa yote zina taa za kuangaza usiku ambazo zinatumia nishati ya jua ambazo zinajiwasha na kujizima zinapohisi giza au mwanga.


Chato imejengeka kama mji ulio tayari kupokea wageni wengi kwani karibu kila mtaa kuna nyumba ya kulala wageni na maeneo mengine katika mtaa nyumba hizo zipo zaidi ya mbili.

Nyumba hizo za wageni zimejengwa zikiwa na sehemu ya baa mighahawa, ili mbali na kulala wageni waweze kula, kunywa na kuburudika.

Hata hivyo, tofauti na ilivyokuwa miaka miwili iliyopita wamiliki wa nyumba hizo wanasema biashara imepungua kwa kiasi kikubwa, tofauti na kipindi Rais wa awamu ya tano akiwa hai.

Wakati huo, wanasema biashara hiyo ilikuwa inafanya vizuri kuliko sasa kwa kuwa wageni wanaotembelea mji huo wamepungua.


“Wakati mzee (Magufuli) anaingia madarakani watu walianza kuongezeka huku na watu walikuwa wakati mwingine wanakosa sehemu za kulala, ndipo baadhi ya watu wakaamua kukimbilia biashara hii.

Mfanyabiashara mwingine katika mji huo, Mallack William alisema Chato ilikuwa inapanuliwa kimkakati na kasi ya ukuaji wake ilikuwa kubwa kiasi ambacho kilipandisha bei ya vitu katika mji huo ikiwemo ardhi ambayo sasa imeanza kurudi chini kama ya zamani.

“Unajua miradi mikubwa ya maendeleo katika mji huu imetawanywa, ukiangalia ulipo uwanja wa ndege, ofisi kuu za Serikali, hospitali ya rufaa na stendi ni mbalimbali, lengo lilikuwa ni kukuza mji haraka, wageni walikuwa wengi katika mji huu na bei ya ardhi karibia maeneo yote ilipanda mara dufu,” alisema.

William ambaye amefanya biashara mjini Chato  kwa zaidi ya miaka 10, anasema kabla ya Magufuli kuchaguliwa kuwa Rais, Oktoba 2015 ardhi ya mita za mraba 600 ambayo inatosha kwa ujenzi wa nyuma ya kawaida ilikuwa chini ya Sh5 milioni lakini baada ya Magufuli kuwa Rais, Novemba 5, 2015 ilipanda thamani na kufikia Sh15 milioni.


Watumishi wa Serikali na hasa ambao walikuwa wakifanya kazi kwa karibu na Rais Magufuli walianza kununua ardhi huku kwa bei kubwa kwa ajili kujenga nyumba za biashara na za kuishi, lakini pia ofisi za taasisi tofauti nyingi zilifunguliwa huko, hivyo kukawa na wageni wengi wanaohitaji ardhi.

“Sasa hivi viwanja vilivyokuwa vikiuzwa Sh10 milioni vinauzwa Sh6 milioni hadi Sh4 milioni, bei ya ardhi imeporomoka matumaini yaliyokuwa yamebaki ni iwapo Chato ingekuwa mkoa lakini kukwama kwake huenda kukaendelea kushusha thamani ya ardhi katika mji huu,” alisema.

William alisema wengi waliotoka mikoa ya mbali wakanunua viwanja katika mji huo, wamevitelekeza na wengine walikuwa wameshaanza ujenzi lakini kasi imepungua na wengine ni kama vile hawana nia ya kuviendeleza.

“Nyumba zote unazoziona za kifahari zimejengwa baada ya Magufuli kuwa Rais, zamani huku ghorofa lilikuwa kwa Mzee (Magufuli) tu, lakini sasa hivi ona kuna nyumba nyingi za kuishi za ghorofa na hazina watu au zimepangishwa kwa gharama ndogo tu.

“Hapa Sh80,000 unapanga nyumba nzima ya kisasa vyumba viwili vya kulala na sebule,” alisema.


Dickson Chigenge ambaye anaendesha pikipiki katika mji wa Chato naye anasema mara ya mwisho kupata kiwango kikubwa cha fedha ilikuwa ni wakati wa msiba wa Magufuli na tangu wakati huo hajawahi kupata fedha sawa na hizo.

“Wakati wa msiba watu walikuwa ni wengi Chato kuna siku nililala na Sh120, 000 kabla ya hapo kwa siku nilikuwa napata Sh30, 000 Mzee (Magufuli) akiwepo hadi Sh50, 000 lakini sasa ukijitahidi sasa Sh25, 000,” alisema Chigenge.

Chigenge anasema kwa ufupi mzunguko wa watu ndani ya Chato umepungua sana kwa kiasi kikubwa akitolea mfano maeneo ya ufukweni akisema kabla ya kifo cha Rais Magufuli, Machi 17, 2021 siku za mwisho wa wiki watu wengi walikuwa wanatembelea fukwe na huko walikuwa wananunua vitu.

Aliongeza hata kwenye baa wateja wamepungua kwani awali wateja wengi walikuwa ni wa kwenda na kutoka maeneo ya starehe lakini hivi sasa ni mpaka siku za mwisho wa juma napo ni kwa baa chache.

Rosemary Simon ambaye yeye anamiliki mgawaha wa chakula,  anasema wateja wa chakula wamepungua hususani wageni na wateja waliobaki sasa ni wale wa kujirudia (wafanyabiashara wa karibu na mgahawa.

“Magufuli alipokuwapo nilikuwa nauza hadi Sh300,000 kwa siku, wateja wanakuwa wengi mpaka wanakosa pa kukaa, lakini sasa hivi nauza Sh120,000 hadi Sh160,000,” alisema.

Kauli ya Mkuu wa Wilaya

Mkuu wa Wilaya ya Chato, Deusdedith Katwale aliliambia Mwananchi kwa miundombinu iliyopo, ukuaji wa uchumi kwa kasi unaweza kuendelea katika wilaya hiyo chini ya uongozi wake.

“Kuna uwanja wa ndege mkubwa, hospitali kubwa, stendi ya kisasa, minada ya mifugo na taasisi nyingi zipo zinaendeleza ofisi na matawi yake, Mfano kuna Veta Geita, Chuo kikuu cha Dar es Salaam wanafungua tawi huku, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) yote hiyo itachangamsha uchumi wa eneo hili,” alisema.

Alisema miradi yote katika wilaya hiyo inatekelezwa kama ilivyopangwa na kuna mingine itakamilika hivi karibuni na itakapokamilika watu watakuwa wakizifuata huduma.

“Mipango yangu ni kuendelea kukuza shughuli za kiuchumi katika wilaya hii, mwelekeo sasa hivi ni kuweka nguvu katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji, tuna kila sababu ya kufanikiwa katika hilo, ‘‘ alisema.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad