CHADEMA yamshauri Rais Samia kuhutubia Taifa kuhusu Bandari

 

CHADEMA yamshauri Rais Samia kuhutubia Taifa kuhusu Bandari

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemsihi Rais Samia Suluhu Hassan kulihutubia Taifa kuwaondolea wananchi hofu na maswali yasiyo na majibu kuhusu mkataba wa uwekezaji bandarini.


Ombi hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati wa kongamano la wanachama wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha) mjini Geita jana Julai 6, 2023.


Ingawa hakuna sheria wala kanuni inayoelekeza Rais kuhutubia Taifa kutoa ufafanuzi au kuzungumzia masuala yanayoibua mijadala, mara kadhaa Watanzania wamewashuhudia wakuu wan chi wakijitokeza hadharani kuhutubia Taifa kuweka mambo sawa au kutoa muongozi wa mijadala mbalimbali nchini.


Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamini Mkapa alijiwekea utaratubu wa kulihutubia Taifa mara moja kila mwezi; utaratubu ulioendelezwa na Jakaya Kikwete aliyepokea kijiti cha uongozi katika Awamu ya Nne; na hata Hayati John Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano naye alitumia hotuba zake kadhaa kwa Taifa kufafanua masuala mbalimbali muhimu.


Tangu aingie madaraka Machi, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan naye amehutubia Taifa katika matukio na maeneo kadhaa akitoa maelekezo, miongozo na ufafanuzi wa masuala mbalimbali.


Akifafanua ombi na ushauri wake, Mnyika amesema licha ya baadhi ya viongozi wa Kitaifa kuanzia Mawaziri na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufafanua masuala kadhaa kuhusu mkataba huo, umma wa Watanzania bado unaonyesha hofu kuhusu baadhi ya vifungu vya mkataba huo kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai kupitia kampuni ya DP World.


Amesema hofu hiyo ya umma unaongeza umuhimu wa Rais Samia ambaye ndiye Kiongozi Mkuu wa Taifa kujitokeza na kuhutubia Taifa kutoa ufafanua yote yanayoibua sintofahamu.


Ametaja cha 23 cha mkataba huo kuwa miongoni mwa vifungu vyenye utata na vinavyojadiliwa na makundi mbalimbali kwa sababu hakielezi ukomo wa uwekezaji huo.


Kiongozi huyo wa Chadema amesema suala la kampuni ya DP World kupata fursa ya kuwekeza kwenye bandari za Tanzania bila kupitia mcakato wa zabuni kama sheria inavyoelekeza ni eneo lingine tata linalohitaji ufafanuzi kutoka kwa Mkuu huyo wa nchi.


Mnyika amedai ufafanuzi kadhaa unaotolewa na viongozi wa Serikali wakiwemo mawaziri wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, bado haujakidhi kiu ya Watanzania.


Katika matukio na majukwaa tofauti, Waziri Mkuu amekaririwa akisema nia ya Serikali katika makubaliano hayo yaliyoidhinishwa na Bunge ni njema na itanufaisha Taifa huku akiahidi kuwa maoni na mapendekezo ya wadau yanayoendelea kutolewa kwa njia mbalimbali yatazingatiwa.


Katika orodha ya wanaotetea mkataba huo yumo pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi ambaye Juni 26, 2023 video yake fupi ilisambazwa kupitia mitandao ya kijamii akielezea masuala mbalimbali ikiwemo hoja ya ukomo wa mkataba akisema madai kuwa utadumu kwa miaka 100 hayana msingi na hayamo.


Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Nshala Rugemeleza, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, viongozi wa dini na wanaharakati ni miongoni mwa Watanzania waliojitokeza hadharani kuonyesha madhaifu kadhaa katika vifungu vya mkataba huo.


Dk Nshala na wanasheria kadhaa wabobevu wameenda mbali kwa kudai mkataba huo umekiuka baadhi ya Ibara za Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad