Dereva Bajaji Mbaroni, Adaiwa Kumuua Mlinzi ofisi ya DC Moshi






Moshi. Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, linamshikilia dereva bajaji, Abdan Abdi, mkazi wa Majengo kwa Mtei, Manispaa ya Moshi, kwa tuhuma za mauaji ya Michael Dastani Ngulizi, aliyekuwa mlinzi ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi.

Mlinzi huyo mwenye umri wa miaka 55, alikuwa ni askari wa Jeshi la akiba (Mgambo), na alifariki dunia Julai 21, mwaka huu baada ya kujeruhiwa na Abdi (21) na hivyo kusababisha kifo chake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema lilitokea Julai 21, saa 6:30 mchana maeneo ya Majengo kwa Mchomba, baada ya mtuhumiwa huyo kukataa kukamatwa kwa kosa la kufanya fujo na kuwatishia ndugu zake.

"Tukio hili limetokea Julai 21, 2023 majira ya saa 6:30 mchana huko maeneo ya Majengo kwa Mchomba, Kata ya Majengo, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambapo marehemu alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali ubavuni na mtuhumiwa huyo," amesema na kuongeza;


"Kufuatia tukio hili, tunamshikilia Abdan Mohamed Abdi, (24), dereva bajaji kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Michael Dastani Ngulizi, (55), askari wa Jeshi la Akiba (Mgambo) ambaye pia ni mlinzi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi,"

Kamanda Maigwa amesema baada ya tukio hilo kufanyika mlinzi huyo alikimbizwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi, kwa matibabu zaidi ambapo alifariki dunia wakati akiendelea na matibabu.

"Mtuhumiwa baada ya kutenda tukio hili alikimbilia mkoani Tanga ambapo kupitia taarifa za raia wema Jeshi la Polisi tumefanikiwa kumtia mbaroni.”


Kamanda Maigwa amesema chanzo cha tukio ni mtuhumiwa kukataa kukamatwa kwani alikuwa anatafutwa kwa kosa la kuwatishia maisha ndugu zake na kufanya fujo.

Aidha, Kamanda Maigwa ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kutii sheria bila shuruti na kuheshimu vyombo vya dola.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad