Wakati akiwa nyumbani Tanzania kwa mapumziko mafupi mara baada ya msimu wa Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia kumalizika, faili la Simon Msuva limetua kwenye meza ya nyota wa zamani wa Liverpool, Manchester City na timu ya taifa la England, Robbie Fowler.
Siku chache zilizopita lijendi huyo wa Kiingereza ambaye ni mshindi wa UEFA Cup mwaka 2000–01 na UEFA Super Cup 2001 akiwa na Liverpool alitangazwa kuwa kocha mpya wa chama hilo ambalo msimu uliopita mfungaji wake bora ni Msuva akiwa na mabao manane.
Al-Qadsiah aliandika kwenye mitandao yao ya kijamii: "Robbie Fowler. Mmoja wa wachezaji maarufu katika Liverpool na Ligi Kuu ya Uingereza. Ni Kocha wa Qadisiyah."
Al-Qadsiah ilimaliza katika nafasi ya 11 katika Ligi Daraja la Kwanza huko Saudi Arabia msimu uliopita wakiwa na pointi 23 nyuma ya nafasi nne za juu za kupanda Ligi Kuu ya Saudia.
Fowler ambaye enzi zake alikuwa mshambuliaji, anakibarua cha kuzungumza na baadhi ya nyota wa timu hiyo akiwemo Msuva kuhakisha wanaongeza mkataba wa kuendelea kuipigania timu hiyo kupanda daraja. Kwa upande wake Msuva alisema ameona uteuzi huo lakini kwa upande wake anatazama zaidi ofa nzuri ambayo itawekwa mezani.
"Bado hajanitafuta na pengine kwa sababu kila kitu changu kipo kwa watu ambao wananisimamia, naamini kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho tutawasikiliza kabla ya kufanya maamuzi mengine," alisema.
Kwa sasa kumekuwa na wimbi la wachezaji na makocha mbalimbali kutoka barani kukimbilia Asia kwa ajili ya kuvuna pesa za Waarabu kama vile Karim Benzema, N'Golo Kante na Ruben Neves wakiwa miongoni mwa waliomfuata kipindi hiki mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Cristiano Ronaldo kwenda Mashariki ya Kati.