Dar es Salaam. Mashabiki na wapenzi wa Yanga wamekaa mkao wa kula kusikilizia hatma ya straika na Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita na Kombe la Shirikisho Afrika, Fiston Mayele ambaye inaelezwa jana alitarajiwa kukutana tena na mabosi wa Yanga kukata mzizi.
Mayele alifunga mabao 17 na kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu, huku akifunga mabao 14, yakiwamo saba ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo Yanga ilifika fainali mbali na mengine saba aliyotupia kwenye mechi za awali za Ligi ya Mabingwa.
Sasa sikia, kama kuna kitu kinawapasua vichwa mabosi wa Yanga ni ofa za straika huyo zilizopo mezani mwao na kwamba wiki hii inayoanza leo anaweza kuuzwa nje ya nchi kutokana na ofa hizo nono zinazowatoa udenda mabosi hao.
Kwenye meza ya mabosi wa Yanga kuna ofa za fedha nyingi tatu, lakini kubwa ambayo imeshtua ni ile ya Pyramids na Misri na nyingine kutoka Saudi Arabia zinazowapa ugumu mabosi wa Yanga kumbakisha kikosini mshambuliaji huyo.
Iko hivi. Ingawa mabosi wa Yanga wamekuwa wakifanya siri kubwa, lakini uhakika ni kwamba klabu hiyo imepokea ofa ya kufuru ikiwamo ofa ya Dola 600,000 (zaidi ya Sh 1.4 Bilioni), huku vurugu za kugombea saini hiyo zikiendelea kwa kasi hatua iliyoongeza presha kubwa kwa mabosi wa klabu.
Yanga inataka kumbakisha Mayele, lakini ofa hizo zinaleta ugumu licha ya mshambuliaji huyo aliyewekwa fedha ndefu na klabu huku akikomalia kutaka aachwe akatafute changamoto mahali pengine baada ya misimu miwili Jangwani.
Endapo Mayele (29) atasimamia msimamo wa kuondoka Yanga anaweza kujikuta anavuna mshahara wa dola 75,000 kwa mwezi (zaidi ya Sh 83 milioni), hatua itakayomweka katika ugumu kukubali kusalia klabu hiyo, licha ya mapenzi yake mbele ya timu hiyo.
Kwa mwaka mmoja tu, iwapo atakubaliana na ofa hiyo itamfanya avune jumla ya Dola 900,000 (zaidi ya Sh2.1 Bilioni) kiasi ambacho kinampasua kichwa akiomba mabosi wa Yanga kumkubalia ofa hizo ili kama mambo yasipoenda sivyo huko, basi atarudi nchini.
“Mayele anaona sasa umri wake huu ni bora kuchukua fedha hizo, ili atengeneze maisha, kwani hiki ndio kipindi cha kupata fedha hizo, anajua Yanga wanampenda na ana furaha kuwa nao, ila ni muhimu kuangalia maisha ya baadaye,” alisema mmoja wa mabosi wa Yanga na kuongeza;
“Ofa zimekuwa nyingi sana na zinaendelea kumiminika hasa baada ya kuwa katika kinyang’anyiro cha kuwania mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani, hivyo presha ya kuondoka kwetu ni kubwa na lolote linaweza kutokea wiki hii.”
Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba mabosi wa klabu hiyo wanaweza kutoa msimamo, wiki hii juu ya ofa ipi wataichukua baada ya kuzungumza na klabu kadhaa ambazo zimefika mezani kwao.
Yanga pia kwa akili nyingine imeshaanza mchakato wa siri wa kutafuta mshambuliaji mwingine ikiwa ni maandalizi iwapo Mkongomani huyo ataondoka klabuni hapo.
Mayele katika miaka miwili aliyokaa Yanga amefanikiwa kufunga jumla ya mabao 33 kwa misimu miwili ya ligi ya ndani akiibuka mfungaji bora msimu huu mbali na mabao mengine kwenye Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho ASFC, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika hatua nyingine kocha mkuu mpya wa Yanga, Miguel Gamondi ameanza kupitia mafaili ya wachezaji wa timu hiyo kabla ya kufanya maamuzi, ikiwa ni saa chache tangu atue nchini na kukutana na viongozi wa klabu hiyo.