Hili Hapa Tatizo Jipya Timu ya Simba

 

Hili Hapa Tatizo Jipya Timu ya Simba

Zimebaki siku 12 tu kabla usajili wa Ligi Kuu Bara haujafungwa baada ya kufunguliwa mwanzoni mwa mwezi huu.


Umekuwa usajili wenye pilikapilika nyingi kwa timu kadhaa huku nyingine zikiwa kimya kama vile hakuna jambo lilotokea au linaloendelea, haya ndiyo maisha ya soka yalivyo Afrika na hata Ulaya.


Timu kubwa za Simba, Yanga na Azam zimeonekana kuwa kwenye kasi nzuri huku zikishusha majembe kadhaa makubwa kwa ajili ya kuhakikisha msimu ujao wanakuwa na timu bora zaidi ya ile iliyopita.


Kwa upande wa Simba hadi sasa wameshasajili wachezaji sita, watano wa nje ambao ni Fabrice Ngoma ambaye anacheza nafasi ya kiungo, Willy Onana anayecheza ushambuliaji, Kramo Aubin ni winga, Che Malone Fodoh anayecheza beki wa kati na mzawa mmoja, David Kameta anayecheza beki wa kulia, lakini kukiwa na taarifa inaweza kuongeza wengine kabla dirisha halijafungwa rasmi.


Kwa picha ya haraka, inaonekana Simba inapambana kutafuta jinsi ya kuziba mapengo ambayo yaliyoisumbua msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Bara, Kombe la Azam Federation na hata michuano ya kimataifa.


Msimu uliopita Simba ilikuwa ndio timu kwenye Ligi Kuu Bara iliyofunga mabao mengi kuliko nyingine 15 zilizoshiriki ligi hiyo, pia ilitoa mfungaji bora baada ya Saido Ntibazonkiza kufunga mabao 17 msimu mzima akifungana na Fiston Mayele wa Yanga.


Kwa haraka unaweza kuona Simba haikuwa na shida kubwa eneo la ushambuliaji lakini bado ilitakiwa kufanya usajili ili kulinda zaidi kama lolote linaweza kutokea, basi wawe na uwezo wa kupata mbadala.


Msimu uliopita, tatizo la mchezaji mmoja kwa Simba lilikuwa linaonekana kuathiri kikosi moja kwa moja na ilikuwa ngumu kwao kupata ushindi kwenye michezo kadhaa kutokana na kukosekana mchezaji mmoja au wawili.


Hata hivyo, pamoja na Simba kufanya usajili huo inaonekana kuna sehemu muhimu ambazo timu hiyo imeshindwa kuzigusa na hivyo wanaweza kushindwa kutimiza malengo yao pamoja na nguvu kubwa ambayo wanaonekana kuitumia kwenye usajili huu hadi sasa.


KIPA


Moja ya mambo yaliyoikwamisha Simba kutwaa angalau taji moja msimu uliopita, ni kukosa kipa wa kiwango cha juu kwenye michezo ya mwishoni mwa msimu.


Simba imekuwa ikimtegemea Aishi Manula kwa zaidi ya miaka mitano sasa na msimu uliopita alishindwa kuumalizia kutokana na majeraha ya nyama za paja.


Hii ilimlazimisha kocha wa timu hiyo, Olivier Robert Robertinho kumtumia kipa namba tatu, Ally Salim baada ya uongozi kuwa na shida na Beno Kakolanya.


Hili lilisababisha Simba iondolewe kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Azam Federation ilipocheza na Azam FC kwa mabao ambayo yanaonekana dhihiri kungekuwa na kipa mwenye uzoefu labda timu hiyo ingevuka.


Kwa michuano hiyo, hali halisi ilionyesha kutokuwa na kipa mwenye uzoefu wa kutosha kulichangia kwa sehemu kubwa timu hiyo kuondolewa.


Kwa msimu huu, hadi sasa zikiwa zimebaki siku 12 dirisha la usajili lifungwe, Simba pamoja na kusajili wachezaji wengine sita, lakini bado haijasajili kipa itakayomtumia kwenye michezo ya mwanzoni mwa msimu ujao kabla Manula hajarejea uwanjani rasmi.


Hii inaonyesha Simba inaweza kumpata kipa bora lakini itawalazimu kumsubiri kwa michezo kadhaa ili aweze kuzoeana na mabeki wake, lakini ni dhahiri timu hiyo itatakiwa kumweka nje kwanza ili aendelee na mazoezi ya kujiweka sawa na msimu kwa kuwa timu nyingi za Afrika bado hazijaanza maandalizi rasmi ya msimu mpya wa ligi na hivyo kama atakuwa anatoka nje atakuwa mmoja wa watu hawa.


Ni sahihi kama Simba wangekuwa na kipa wao kwa sasa kwenye maandalizi ya msimu kwa kuwa angetumia muda huo kujiandaa lakini kuzoeana na wachezaji wenzake ili kufahamu watacheza vipi kwenye ligi na michuano mingine ambayo watashiriki. Au wakubali wataanza msimu na Salim kama ambavyo walimaliza naye, ataweza mikikimikiki kweli, tusubiri.


KWA TSHABALALA MAMBO MAGUMU


Simba imefanya vizuri kwenye eneo la usajili kwa kipindi cha hivi karibuni, ingawa kwa baadhi ya sajili walifeli.


Msimu huu bado hadi sasa hawajafunga usajili wao ingawa inaonekana kutakuwa na tatizo kwenye kikosi chao.


Tayari imeshamsajili beki mmoja wa kulia, David Kameta Duchu atakayeungana na Shomary Kapombe na Israel Mwenda, huku hakuna shida kwa kuwa ni utamaduni wa Simba kuwatumia wazawa kwenye upande huu wa ulinzi, lakini upande wa kushoto ambapo pia wamekuwa wakitumika wazawa bado kunaonekana kuwa na tatizo.


Ni sahihi kwa atakayesema Kapombe na Tshabalala wamecheza wenyewe kwa muda mrefu, hivyo wanaweza kuamini na msimu ujao watacheza tena, lakini ni kamari ya pata potea.


Wengi wanaamini Mwenda anaweza kucheza upande wa Tshabalala, sawa, lakini swali la kujiuliza beki huyo alikosa nafasi wakati anacheza kwenye sehemu yake ya asili, upande wa kulia, kwa nini leo inaaminika anaweza kuwa bora upande wa kushoto?


Simba ili wafanya vizuri kwenye ligi na michuano mingine ambayo itashiriki msimu ujao ikiwemo ile ya Super Cup inalazimika kusajili beki mmoja wa kushoto au wawili ikiwa na maana kama Tshabalala atapata majeraha au shida nyingine basi huyo atakayesajiliwa anaweza kuziba pengo lake.


Lakini hata kama wana mpango wa kufanya hivyo, hili ni jambo lililotakiwa kufanyika mapema ili kumpa mchezaji huyo nafasi ya kwenda kujiandaa na wenzake kwenye maandalizi ya msimu Uturuki na kumpa nafasi kocha wao kuona kama amefanya chaguo sahihi au la.


Ni ngumu kwa beki mpya atakayekuja kukutana na kikosi Dar es Salaam au atakayekaa kambini chini ya siku 10 kuwa kwenye kasi inayotakiwa, bali atalazimika kusubiri kwa muda ili kuendana na kasi ya wenzake kikosini, hii ikiwa na maana kuwa anaweza kukosa michezo ya mwanzoni mwa msimu.


WACHEZAJI MASTAA KUCHELEWA


Siyo jambo geni kwenye soka duniani kwa baadhi ya wachezaji mastaa kuchelewa kuungana na wenzao kwenye kambi ya mazoezi hata Ulaya imekuwa ikitokea mara kwa mara.


Lakini mara nyingi wale ambao wamekuwa wakichelewa kujiunga na wenzao kwenye maandalizi ya msimu huwa hawachezi mechi za mwanzoni kwa kuwa wanakuwa hawako fiti kwa asilimia 100.


Hii ina maana, kocha wa Simba Robertinho atalazimika kujiuliza mara mbili kama atamtumia kiungo wake Clatous Chama kwenye michezo ya mwanzoni mwa msimu ikiwemo ile ya Ngao ya Jamii, pamoja na Willy Onana, Kramo na Che Malone ambao walijiunga na wenzao juzi. Inawezekana wakaendana na wenzao kwa kasi inayotakiwa lakini siyo ajabu kama watachelewa kuwa kwenye ubora wao kwenye michezo ya Ngao ya Jamii mapema mwezi ujao.


MABEKI WA KATI DUH!


Simba imefanya usajili wa beki mmoja wa kati, Che Malone, huku ikiachana na Joash Onyango aliyetimkia Singida Fountain Gate.


Sio usajili mbaya, lakini kama ndiyo wamefunga wanaacha maswali mengine mengi, hii ina maana Simba wana mabeki wakati watatu Inonga, Kenedy Juma na Malone, swali kubwa ni Malone ataweza kuendana na kasi ya Ligi Kuu Bara kwa haraka au atafeli kama ilivyokuwa kwa Mohamed Ouatarra?


Kama akifeli baada ya msimu kuanza na dirisha la usajili kufungwa, ina maana Simba itakuwa imetengeneza tatizo eneo lao la ulinzi kwa kuwa haitakuwa na mtu mwingine imara wa kumpata kwa wakati huo labda wasubiri hadi usajili wa Junuari.


Lakini hata kama ataendana na kasi, ni wazi Simba itatakiwa kuwa na beki mwingine imara wa kati ili mmoja wao kati ya Malone na Inonga akipata majeraha, achukue nafasi zao nah ii ilikuwa kwa Kennedy msimu uliopita.


MICHUANO MITANO


Simba itashiriki kuwania makombe matano msimu huu, Ngao ya Jamii itakayochezwa kwa mfumo wa ligi, Ligi Kuu Bara, Kombe la Azam Federation na Super League ya Afrika na Ligi ya Mabingwa Afrika.


Michuano hii inawalazimisha kuwa na kikosi kipana na chenye wachezaji wengi vijana watakaocheza michezo mingi bila kuchoka.


Kusajili wachezaji wengi wakongwe kunaweza kuwarudisha nyuma Simba kwani ni dhahiri watachoka mapema, hivyo kwa muda ulibaki Simba wanatakiwa kuhakikisha wanasajili wachezaji wenye umri mdogo watakaokimbizana na kasi ya michuano yote msimu huu na mingine ijayo.


KOCHA KUONDOKA KAMBINI


Linaweza lisiwe tatizo kubwa kwa kuwa ana wasaidizi wake ambao wanaendelea na kazi lakini inapunguza kasi ya mastaa wake kama hawatawapa heshima wale waliobaki.


Ni wazi hakukuwa na ulazima wa kwenda Brazil kuendesha kozi kama ilivyoripotiwa na angeendelea na maandalizi ya kikosi chake hadi mwishoni ndio aende kumalizia mafunzo yake.


Kitendo cha kuamini anaondoka kwa kuwa ana wasaidizi wanaoweza kufanya kazi zake sio sahihi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad