Menejimenti ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imetoa ufafanuzi kuhusu uvunjifu wa maadili uliofanywa na Mgonjwa (jina limehifadhiwa) na anayedaiwa kuwa Mpenzi wake (jina limehifadhiwa) ndani ya wodi (3A) siku ya Jumapili mchana tarehe 9/07/2023 ambapo katika uchunguzi wa awali mgonjwa amekiri kufanya tendo la busu la midomo na ndimi na Mpenzi wake katika mazingira ya kuumwa ndani ya Hospitali kitu ambacho ni kinyume cha maadili ya kitanzania.
“Menejimenti imebaini kwamba Mpenzi wa Mgonjwa huyo si Mtumishi wa Taasisi ya MOl, aidha tukio hilo liligunduliwa na Muuguzi aliyekuwepo wodini ambapo alichukua hatua ya kuzuia Wahusika kuendelea na kitendo hicho, Menejimenti inaendelea kuchukua hatua zaidi kwa Wahusika”
“Uchunguzi zaidi umebaini pia wakati vitendo vinaendelea kuna Mgonjwa jirani (jina linahifadhiwa) ambaye alisharekodi video, Menejimenti ya MOl inalaani kitendo hicho cha uvunjifu wa maadili kilichofanywa na Mgonjwa huyo pamoja na Mpenzi wake, vilevile Menejimenti inalaani na kukemea kitendo cha kurekodi video wodini na kutuma kwenye mitandao ya kijamii kilichofanywa na Mgonjwa jirani”
“Matukio haya yote ni kinyume na mwongozo wa Wizara ya Afya unaozuia kufanya matendo ya uvunjifu wa maadili kwa mgonjwa na kurekodi video wodini, Menejimenti inaendelea kuchunguza zaidi tukio hili ili kujiridhisha kuwa hapakuwa na uzembe katika kusimamia usalama wa Wagonjwa wakati Ndugu wanawatembelea Wagonjwa wodini” ——— MOI.