Unguja. Hoteli nne na nyumba moja ya makazi zimeungua moto Paje Wilaya ya Kusini Unguja, Mkoa wa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Hoteli hizo ni pamoja na; Cristal resort, Maisha Matam, Drifters na The Nest Boutique resort
Mkuu wa Wilaya hiyo na Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, Rajab Mkasaba ameileza Mwananchi Digital kuwa tukio hilo limetokea saa 6:00 usiku wa kumkia leo Julai 9, 2023.
"Kuna hoteli nne na nyumba moja ya kulala wageni hapa Paje zimeungua sehemu ya reception (mapokezi) kutokana na moto, baadhi ya wafanyakazi wanasema moto umeanzia jikoni lakini bado uchunguzi unaendelea," amesema Mkasaba
Amesema hakuna aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa katika ajali hiyo na kwamba moto huo umeenea kwenye hoteli zote hizo kwasababu ya upepo na ikizingatiwa zimeezekwa kwa makuti.
Mkasaba amesema wananchi kwa kushirikiana na jeshi la zimamoto wamefanikiwa kuzima moto huo bila kuleta madhara zaidi.
"Serikali itahaikikisha ulinzi unaimarishwa na huduma muhimu zote zinapatikana bila kuleta adha kwa wageni," amesema.
Leo Jumapili Julai 9, 2023 saa 3.00 asubuhi akiongea na Mwananchi Digital Kamanda wa polisi mkoa huo, Gaudianus Kamugisha amethibitisha kutokea ajali hiyo na akiahidi kutoa taarifa zaidi baadae.
“Ni kweli tukio lipo nami nipo na kamati ya ulinzi na usalama ndio tupo njiani tunaelekea eneo la tukio bado sijapata taarifa kamili kuna askari wangu ndio wapo eneo la tukio, taarifa zaidi nitakupa baadaye," amesema.