Rais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk Jakaya Kikwete
ais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk Jakaya Kikwete
Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa anajivunia jinsi Rais Samia Suluhu anavyoongoza nchi kwa utulivu licha ya changamoto anazopitia.
Kikwete ameyasema hayo jioni ya leo julai 18, 2023 jijini Arusha, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa mwaka wa Jukwaa la Demokrasia Unaoangazia Masuala ya Uongozi barani Afrika, ulioandaliwa na taasisi za MS-TCDC (Tanzania), Center for Strategic Litigation (Tanzania), na Institute for Security Studies (Afrika Kusini).
Amesema kuwa Rais Samia alianza kumvutia kwenye usuluhushi wa mgogoro wa Zanzibar baada ya uchaguzi wa mwaka 2000, ambao alifanikiwa kuuona upeo wake mkubwa katika uongozi baada ya kuwa kwenye kamati moja ya uchaguzi na usuluhishi juu ya mgogoro huo.
"Baada ya mgogoro ule tuliundwa timu moja kuzunguka sehemu mbalimbali duniani kuelezea kilichotokea na kupata azimio kuwa usuluhushi bora utatokana na mazungumzo," amesema Kikwete
Kw amujibu wa Rais huyo wa awamu ya nne, mchango wa Rais Samia katika vikao vyao vilimpa umakini juu yake na baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kushika nafasi ya Urais, hakuweza kumuacha nyuma katika baraza lake la mawaziri, ili aweze kuvuna upeo wake katika uongozi.
"Baadae mwaka 2005 baada ya kuchaguliwa, nilimkumbuka Rais Samia na kumteua katika nafasi ya uwaziri wa nchi, Ofisi ya Rais Muungano na Mazingira, uzuri hakuniangusha kwani aliifanya kazi yake vema na kuanza kujivunia yeye zaidi," amesema.
Kikwete amesema kuwa hata baada ya kuondoka kwenye nafasi ya Urais, alifanikiwa kumshawishi Rais John Magufuli kumteua Rais Samia kuwa mgombea mwenza na baadaye aalifanikiwa kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke na sasa ni mkuu wa nchi.
"Wakati naongoza nchi nilipitia changamoto nyingi ikiwemo za kashfa mbali mbali za EPA, ESCROW, Richmond na zingine nyingi, lakini niliendelea kuongoza nchi kwa utulivu na kwa ushauri na uzuri yote yakapita," alisema Kikwete.
Alisema kuwa changamoto mbali mbali anazopitia Rais Samia katika uongozi wake ikiwemo mambo yanayoibuka, angepaniki kidogo tu angevuruga watendaji wake na nchi nzima kwa ujumla lakini utulivu unamsaidia licha ya hasira alizonazo.
"Rais Samia kufanikiwa kufikia leo ni utulivu pekee unamsaidia, maana hakuna nafasi ngumu kama aliyonayo lakini kwa sababu ya utulivu wake ingawa ana hasira lakini mambo yanaenda, hiyo pekee inatosha mimi kujivunia yeye baada ya kumuibua huko Zanzibar na kumleta Muungano," amesema.