Kina Mdee, Katiba Mpya vyazua Jambo Chadema

 

Kina Mdee, Katiba Mpya vyazua Jambo Chadema

Mvutano wa ama kuendelea au kutoendelea na mazungumzo ya maridhiano umeibuka ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu kutofautiana kimtazamo.


Habari za kuaminika zinadai kuwa kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kilichokutana Julai 8, pamoja na mambo mengine kilijadili mwenendo wa mazungumzo kati ya chama hicho na Chama cha Mapinduzi (CCM).


Katika mazungumzo hayo, Chadema inaongozwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe akiwa na Katibu Mkuu, John Mnyika, mjumbe wa Kamati Kuu, John Heche; mwanasheria wa chama, Jeremiah Mtobesya, Tundu Lissu (Makamu Mwenyekiti- Bara) na mjumbe wa kamati kuu kutoka Zanzibar, Zuedi Mvano.


CCM kwa upande wake kinaongozwa na Makamu Mwenyekiti (Bara), Abdulrahman Kinana, aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge na Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene.


Wajumbe Chadema wagawika


Chanzo chetu katika kikao hicho kilieleza kuwa miongoni mwa hoja zilizochukua muda mrefu kujadiliwa na wajumbe wa Chadema, ni mwenendo wa maridhiano huku wajumbe wakigawika pande mbili.


Kulikuwa na upande uliotaka mazungumzo yaendelee, huku mwingine ukitaka chama kijitoe, kwa madai ya kusuasua kwa utekelezaji wake hasa eneo la Katiba mpya na uwepo wa wabunge 19 bungeni ambao chama hicho kiliwafukuza uanachama.


Baadhi ya wajumbe hao waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina, walisema hoja hiyo ilikuwa na mvutano kutokana na mazingira mbalimbali ya kisiasa yalivyo kwa sasa nchini.


“Tulijadili kwa kina suala hili la maridhiano, wapo waliotaka tujitoe kwa sababu hawaoni dalili njema huko mbele, bali ni kupotezeana muda, twende kujenga chama,” kilieleza chanzo hicho na kuongeza:


“Baada ya mjadala mrefu, tulikubaliana tusimame kwanza kuendelea na vikao vile, yaani timu ya Chadema na ile ya CCM na kumwomba Mwenyekiti (Mbowe) kukutana na Mwenyekiti mwenzake wa CCM (Rais Samia Suluhu Hassan) ili kufahamu kwa nini baadhi ya mambo hayaendi.”


Mjumbe mwingine alisema maridhiano hayo yamekuwa na matunda licha ya kusuasua; ikiwemo kurejeshwa kwa mikutano ya hadhara, kesi nyingi za kisiasa zikifutwa na mchakato wa Katiba kufufuliwa.


“CCM imekubali na vikao vyake vya juu kabisa vikaunga mkono, hivyo hatuna budi kupongeza hili, lakini kama tulivyosema kwenye vikao vyetu kuna mambo hayako sawa. Wale wabunge 19 kule bungeni hawawakilishi Chadema, sasa wanafanya nini. Katiba mpya nayo vipi, mbona imekuwa danadana tu?” alihoji mjumbe huyo.


Kwa sasa sakata la wabunge hao lipo kwenye vyombo vya sheria ambapo, Bunge linasubiri maamuzi ya mahakama kwa hatua zaidi.


Kuundwa kamati maalumu


Habari zaidi kutoka ndani ya chanzo chetu zimeeleza kutokana na mvutano huo na hofu ya baadhi ya wajumbe, kamati kuu iliazimia kuundwa kwa kamati maalumu itakayokuwa chini ya Mnyika, ikiwahusisha pia Reginald Munisi (Mkurugenzi wa Uchaguzi), wanasheria Jonathan Mndeme na Mtobesya.


Kamati hiyo itakuwa na jukumu la kufanya uchambuzi na tathimini ya kina ya hoja zote zilizoibuliwa wakati wa vikao vya maridhiano na kukubaliana kupatiwa ufumbuzi.


Baada ya uchambuzi huo utakaoangazia mambo muhimu yaliyotekelezwa na ambayo yanaonekana kusuasua katika maridhiano hayo, itatoa mapendekezo yake na hatua za kuchukuliwa.


Alipotafutwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema kuhusu mitazamo tofauti ya wajumbe kuhusu mchakato wa maridhiano, alisema hana taarifa. “Hakuna taarifa kama hizo, lakini huyo aliyekueleza mwambie akueleze zaidi. Mwenyekiti (Mbowe) hawezi kupewa maelekezo. Narudia sina hizo taarifa na nilikuwa kwenye kikao sina hizo taarifa.”


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema: “Kwa kuwa mwenyekiti (Mbowe) aliahidi kuzungumza atafanya hivyo, wananchi wasiwe na wasiwasi siku bado hazijaisha.


“Kuna ukweli au uongo kutoka hicho chanzo cha habari kwa vile Mbowe alishaahidi mbele ya umma basi atalizungumzia. Kwa sababu hakuna chochote cha ajabu atazungumza tu,” alisema Mwalimu.


Sakata lilivyoanza


Julai 8 mwaka huu, Kamati Kuu ya Chadema iliketi na kutoa msimamo kuhusu sakata la mkataba wa makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na ile ya Dubai ya uwekezaji na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam.


Pia, suala la Katiba mpya na operesheni za chama lilikuwa sehemu ya kikao hicho, huku Mbowe akieleza kuwa maridhiano yanahitaji muda, uvumilivu na kuwahusisha watu wengi zaidi.


Julai 14, mwaka huu, Mbowe akazungumza na wanahabari kuhusu maazimio ya kamati kuu, lakini akaweka pembeni kwanza suala la maridhiano na uhamishaji wananchi kwenye Hifadhi ya Ngorongoro, huku na akijielekeza kwenye sakata la mkataba wa Serikali ya Tanzania na Dubai kuhusu uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.


"Nilikusudia kuzungumza mambo matatu, la kwanza mkataba wa bandari na DP World, maridhiano kati ya Chadema na CCM kuhusu mustakabali wa Katiba Mpya na Taifa na jambo la Ngorongoro na Loliondo.


"Lakini baada ya mashauriano na wenzangu tumeona tukizungumza yote haitakuwa sawa, maana yana uzito unaofanana. Leo (Julai 14) nitazungumzia DP pekee, la Ngorongoro na maridhiano tutalizungumza wiki ijayo,” alisema Mbowe.


Hata hivyo, wakati Mbowe akisubiriwa kuitisha mkutano kuzungumza na wanahabari kuhusu masuala hayo, vyanzo vya kuaminika vimeidokeza Mwananchi kuwa mvutano uliopo ni baadhi ya wajumbe kutoridhishwa na mwenendo wa maridhiano yaliyoanza Mei 20, 2022 Ikulu ya Chamwino, Dodoma chini ya Rais Samia, huku Mbowe akiongoza ujumbe wa chama chake.


Inaelezwa baadhi ya wajumbe wa kamati kuu wanaulalamikia mwenendo wa maridhiano kwa sababu mapendekezo waliyotoa hayatekelezwi kwa ufanisi. Miongoni mwa hayo ni kuondolewa kwa wabunge 19 wa viti maalumu bungeni na kurejeshwa kwa mchakato wa Katiba mpya.


Wabunge hao wakiongozwa na Halima Mdee walivuliwa uanachama Novemba 27, 2020 baada ya Novemba 24, 2020 kuapishwa kuwa wabunge, huku Chadema wakidai hawakupeleka majina ya wabunge wa viti maalumu kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).


“Wakati mchakato wa maridhiano unaanza jambo la awali ambalo tulilitarajiwa kupatiwa ufumbuzi ni kuondolewa bungeni kwa wabunge 19, lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea. Wabunge wale (kina Mdee) hawastahili kuwepo mule ndani, lakini kuna kila dalili hili limeshindikana na sasa tunakaribia uchaguzi.


“Ukiacha hilo, suala la mchakato wa katiba mpya kila siku ni maneno matupu bila vitendo, muda wa uchaguzi unakaribia, sasa tunakwendaje kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa na baadaye uchaguzi mkuu kwa sheria na katiba ya zamani ambazo zimekuwa kikwazo cha haki kwa upinzani,” kilisema chanzo chetu ndani ya vikao hivyo.


Chanzo kingine kimedai kuwa Rais Samia ameonekana kuyapa kipaumbele zaidi mapendekezo yaliyotolewa na Kikosi Kazi alichokiunda kuchunguza masuala mbalimbali, ikiwemo kukwama kwa Katiba mpya.


Kimeeleza kuwa mapendekezo ya Chadema siyo kuanza na tume huru ya uchaguzi, bali Katiba mpya lakini kinachoonekana ni tofauti.


Tayari Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imeviandikia barua vyama kuvitaka kutoa maoni na mapendekezo kuhusu mabadiliko ya sheria nne.


Sheria hizo ni ile ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, Sheria ya vyama vya siasa sura ya 258 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi sura ya 278.


Mchakato huo unafanyika ikiwa ni takribani mwaka mmoja kabla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 na miaka miwili kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.


Kupitia barua hiyo, Ofisi ya Msajili imewataka makatibu wa vyama kuwasilisha maoni kuhusu sheria hizo kabla ya Julai 20, mwaka huu.


Hata hivyo, Chadema kupitia Mnyika ilisema suluhisho lingekuwa ama kuanza na Katiba mpya au marekebisho ya Katiba ya sasa ili kutibu matatizo ya kiuchaguzi.


Chadema ambacho ni chama kikuu cha upinzani, kilishaweka msimamo wake kwamba hakitakubali kuingia katika uchaguzi mkuu ujao kupitia Katiba ya sasa yenye maudhui ya chama kimoja.


Mnyika alisema matatizo ya kiuchaguzi ni ya kikatiba, hivyo marekebisho ya sheria ya uchaguzi hayawezi kuyatatua kabla ya kuanza na ama Katiba mpya au marekebisho ya Katiba ya 1977.


“Kutaka maoni kuhusu marekebisho ya sheria ya uchaguzi ni kurudia kazi ambayo ilishafanywa na kikosi kazi, hivyo ni mbinu ya kuchelewesha kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya,” alisema Mnyika kupitia ujumbe wake wa maandishi.


Aliongeza: “Pia hii ni kukwepesha haja ya kufanyika kwa marekebisho ya mpito ya kikatiba kuwezesha uchaguzi huru na wa haki. Katika wakati mwafaka, chama kitatoa tamko la kina juu ya hatua hii ya msajili wa vyama vya siasa yenye nia mbaya,” alisema Mnyika.


Kinachotakiwa kufanyika


Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Dk Faraja Kristomus amesema: "Kama haya tuliyosikia kutoka Chadema yana ukweli, basi huenda hali ya kisiasa ikarudi kwenye mvutano kama uliokuwepo miaka ya nyuma.


"Nadhani busara inahitajika kwa pande zote mbili. Upande wa CCM na Serikali yake na upande wa Chadema kama chama cha upinzani chenye ushawishi mkubwa nchini."


Dk Kristomus alisema huenda Chadema wana madai ya msingi baada ya kufanya uchambuzi wao, lakini inapotokea upande mmoja wa maridhiano unaonekana kukiuka makubaliano, upande mwingine una haki ya kulalamika.


"Nafikiri Chadema wanaweza kutumia njia sahihi kufikisha malalamiko. Bahati mbaya hoja zao zinakuja kipindi ambacho nchi inajiandaa kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwakani na uchaguzi mkuu wa 2025.


"Hivyo, Chadema kisipuuzie hoja ya kujiandaa na uchaguzi kwa kuwa wananchi wanahitaji kupata wagombea kutoka vyama tofauti ili wawe na haki ya kuwachagua wanaoona wanafaa," alisema Dk Kristomus.


Amesema Katiba mpya ni muhimu kwa sasa, lakini kuwepo na uchaguzi huru na wa wazi, ni jambo la msingi zaidi. Kwa sasa mchakato huo wa maridhiano unatajwa kuwa kichocheo cha kurejesha amani na uhuru kwa vyama vya siasa, hasa upinzani kufanya shughuli za kisiasa bila bughudha.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad