Beki wa kati ya Timu ya Taifa ya Uganda na Klabu ya SC Villa ya nchini humo, Gift Fred.
IMEELEZWA kuwa Yanga imetumia dau la Sh 200Mil kufanikisha usajili wa beki wa kati ya Timu ya Taifa ya Uganda na Klabu ya SC Villa ya nchini humo, Gift Fred.
Yanga ipo katika mipango ya kukisuka kikosi hicho ili kifanye vema katika msimu ujao ambao wamepanga kufika hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga tayari imekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji wa Singida Fountain Gate, Nickson Kibabage ambaye imenunua mkataba wake kwa Sh 122Mil.
Wakala wa Gift, Ivica Stankovic ameliambia Championi kuwa tayari wamekamilisha mazungumzo kwa mteja wake kukubali kusaini mkataba wa miaka kuitumikia timu hiyo kuanzia msimu ujao.
Taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kutoka Yanga ni kuwa, klabu hiyo imemsajili beki huyo kama mchezaji huru akitokea SC Villa mara baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, beki huyo amesaini mkataba wa miaka mitatu baada ya kutua nchini akitokea nyumbani kwao Uganda kufuatia kufikia makubaliano mazuri kati ya uongozi wa Yanga na menejimenti ya mchezaji.
Aliongeza kuwa usajili huo umefanyika kwa mujibu wa ripoti ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Mtunisia, Nasreddine Nabi aliyowakabidhi viongozi.
“Gift ni kati ya wachezaji tuliokuwa nao katika mipango ya muda mrefu kwa ajili ya kuwasajili baada ya uongozi kujiridhisha na kiwango chake.
“Usajili wake haukuwa mgumu katika kumpata, kwani Aucho (Aucho) ametusaidia katika kumpata kwa kuwa wote ni raia wa Uganda.
“Tumefanikisha usajili wake kwa dau la Sh 200Mil ambalo amelitaka yeye ili usajili wake ukamilike. Bado tunaendelea kukiimarisha kikosi chetu wakati tunajiandaa msimu ujao tunakwenda kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akizungumza usajili wa timu hiyo, Ali Kamwe alisema kuwa: “Yanga tayari tumekamilisha usajili wa wachezaji wote tuliokuwa tunawahitaji, muda sio mrefu tutaanza kuvitangaza hadharani mashabiki wetu wawaone.”
STORI: WILBERT MOLANDI, CHAMPIONI