Dar es Salaam. Hatima ya wakili wa kujitegemea, Fatma Karume kufanya kazi ya uwakili Tanzania Bara bado iko njiapanda baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali shauri lake la kupinga kusimamishwa.
Wakili Karume maarufu kama Shangazi, alisimamishwa kwa muda kutoa huduma hiyo na Mahakama Kuu, uamuzi uliotolewa na aliyekuwa Jaji Kiongozi, Dk Eliezer Feleshi mwaka 2019 kutokana na malalamiko ya ukiukaji maadili ya uwakili yaliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Hata hivyo, Karume alifungua shauri la maombi ya mapitio Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo.
Katika shauri hilo la maombi ya mapitio namba 434 la mwaka 2019, aliiomba mahakama hiyo ipitie na kisha itengue uamuzi huo wa Mahakama Kuu.
Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake wa Juni 27, mwaka huu, ulioandikwa na Jaji Dk Paul Kihwelo kwa niaba ya majaji wenzake wengine wawili waliosikiliza shauri hilo, Augustine Mwarija (Kiongozi wa jopo) na Mwanaisha Kwariko, imetupilia mbali shauri hilo.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo kwa kuzingatia hoja moja ya pingamizi la awali la Serikali kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu kumsimamisha Karume uwakili haukupaswa kupingwa Mahakama ya Rufani kwa njia ya mapitio.
Mahakama hiyo imesema kwa kuwa kifungu cha 22(2) (b) cha Sheria ya Mawakili ambacho Mahakama Kuu ilikitumia kumsimamisha, pia kinaipa mahakama hiyo mamlaka ya kuondoa amri ya kusimamishwa wakili kutokana na maombi ya wakili husika. Kwa mujibu wa uamuzi huo, Karume alipaswa kufungua maombi ya kuondolewa amri ya kusimamishwa katika Mahakama Kuu badala ya kuchagua kufungua shauri la mapitio Mahakama ya Rufani.
"Tunathubutu kusema kwa sababu hizo zilizotangulia zinahitimisha mjadala katika hoja ya nne ya pingamizi la awali ambayo tunaikubali," imesema Mahakama hiyo katika uamuzi huo kwa tafsiri isiyo rasmi na kuhitimisha:
"Kwa kuwa hoja ya nne ya pingamizi peke yake tu inamaliza shauri, kwa hiyo tunaamua kuwa shauri hili halistahili na tunalitupilia mbali kwa gharama."
Karume aliwakilishwa na mawakili Dk Rugemeleza Nshala na Peter Kibatala na wadaiwa waliwakilishwa na jopo la mawakili watatu lililoongozwa na Wakili wa Serikali, Debora Mcharo.
Kwa mujibu wa wakili Nshala, licha uamuzi mwingine uliowahi kufanywa na Mahakama Kuu, mpaka leo bado Karume yuko katika kifungo hicho, kwani uamuzi wa awali haukutengua amri ya kusimamishwa.
Akizungumzia uamuzi huo, Wakili Kibatala alilieleza Mwananchi hatua inayofuata ni kurudi Mahakama Kuu kuwasilisha maombi kuiomba iondoe amri hiyo ya kusimamishwa kwa muda.
"Mwanzoni tuliogopa kwa sababu ile order (amri, ya kumsimamisha) ilikuwa na maelekezo ya ziada, (yaani Msajili kupeleka malalamiko ya AG kwenye Kamati ya Mawakili) kwa hiyo tuliona kama tungerudi pale tungeambiwa kwa nini mmerudi huku wakati amri haijatekelezwa.
"Lakini sasa kwa sababu hayo ndio maelekezo ya Mahakama ya Rufani tutarudi (Mahakama Kuu) mapema tu wiki ijayo (wiki hii). Tunafurahi tutakaporudi hapo hatutegemei mtu aje atubishie kuwa kwa nini mmerudi hapa." Karume alisimamishwa kutokana na kauli alizozitoa kwenye hoja zake za maandishi katika shauri la kikatiba namba 29 la mwaka 2018 lililofunguliwa na Katibu Mkuu wa chama cha ACT wazalendo, Ado Shaibu.
Shaibu alikuwa akipinga kuteuliwa kwa Profesa Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akidai hakuwa na sifa, lakini Serikali ilimwekea pingamizi la awali.
Akijibu pingamizi hilo, Karume alidai Profesa Kilangi bado ni mchanga kitaaluma, hana uwezo wa kusimamia jukumu la uanasheria Mkuu wa Serikali na kwamba amekuwa akiipotosha Serikali katika mambo mengi.
Hivyo Wakili Mkuu wa Serikali aliwasilisha malalamiko Mahakama Kuu, kwamba kauli hizo ni kinyume na kanuni za maadili ya mawakili na kwamba ni kejeli na kashfa ya kudhalilisha ofisi ya AG.
Kutokana na malalamiko hayo, Jaji Feleshi Septemba 20, 2019 alimsimamisha Karume kutoa huduma za uwakili, kusubiri malalamiko dhidi yake kuwasilishwa na kuamuriwa na Kamati ya Mawakili.
Kamati hiyo katika uamuzi wake Septemba 23, 2020 ilimfuta katika orodha ya mawakili baada ya kumtia hatiani.