Pendekezo la mabadiliko hayo lilitolewa na mkufunzi wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger ambaye amekuwa akifanya kazi kama Mkuu wa Maendeleo ya Soka Ulimwenguni wa FIFA kwa miaka minne.
Sheria ya hivi sasa inasema kwamba, mchezaji atakuwa ameotea kama sehemu yoyote ya mwili wake itakuwa karibu na mstari wa goli la wapinzani kuliko mpira ama mpinzani wake wa pili huku mpinzani wa kwanza akiwa ni golikipa.
Hata hivyo, FIFA wamepanga kurekebisha sheria hiyo huku pendekezo la Wenger likitegemewa kubadili tafsiri ya sheria hiyo kutoka sehemu ya mwili ya mfungaji wa bao mpaka kuwa mwili mzima wa mchezaji atakae funga bao ndio kutafsiriwa kama Offside.
Hii inamaanisha kuwa ikiwa sehemu yoyote ya mwili iko nyuma ya beki wa mwisho, mshambuliaji huyo atakuwa Onside, ili kutafsiriwa kama offside itabidi mwili mzima wa mfungaji wa bao uzidi mwili wa mpinzani wa mwisho.
Sheria hii imedhamiria kuwapatia uhuru washambuliaji wakati wa kushambulia nafasi zilizo nyuma ya wapinzani, kwa maana kwa kawaida, mshambuliaji hutumia mikono yake kuonesha mahali anapotaka kukimbia.
Sheria hiyo imepangwa kufanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza nchini Uholanzi, Sweden na Italia.