Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni iliyopo mkoani Dar es Salaam imewatangazia wananchi, taasisi na kampuni zinazomiliki ardhi katika manispaa hiyo kuwa inakusudia kutwaa maeneo yote ambayo yametelekezwa pasipo kupimwa.
Kusudio hilo limetangazwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni, Erasto Kiwale kupitia taarifa yake kwa umma lililotolewa Juni 30, 2023 likiwa na kumbukumbu namba KGMC/PT/A.1/VOLIX/67.
Kwa mujibu wa taarifa hilo, mkurugenzi huyo amewataka wote wanaomiliki ardhi katika manispaa hiyo kufika katika ofisi yake wakiwa na nyaraka zao muhimu za umiliki wa asili wa maeneo.
“Halmashauri inatoa muda wa hiari wa siku 14 tu kwa kila mwananchi mmoja mmoja, taasisi na kampuni kufika kwenye ofisi za manispaa ya Kigamboni. Baada ya siku hizo kwisha, Serikali itachukua hatua nyingine za kisheria,” inaeleza taarifa hiyo ya Kiwale.
Mpango huo wa manispaa ya Kigamboni umekuja wakati Serikali ikifanya jitihada za urasimishaji wa ardhi kwa kupima viwanja na kutoa hati ili kupunguza makazi yasiyo rasmi yanayosababisha ugumu katika ufikishaji wa huduma muhimu kama zimamoto, maji au umeme.