Waziri wa Nishati, January Makamba ameeleza namna alivyotuhumiwa na watu mitandaoni kuwa na biashara ya majenereta kutokana na umeme kukatika huku akikanusha madai hayo na kueleza njia wanazotumia kukabiliana na changamoto hiyo.
“Kuna wakati umeme ulivyokuwa unakatika zilizuka taarifa kwamba kuna biashara ya majenereta tunaifanya, huku wakimtuhumu Mkurugenzi (Maharage Chande) kuwa na duka la majenereta Tanesco, kitu ambacho siyo sawa na tulikubali kuwa wa wazi na wakweli katika umeme ili tutatue changamoto,”amesema Waziri Makamba.
Makamba ameyasema hayo katika Kongamano la Jukwaa la Fikra kuhusu safari ya Shirika la Umeme (Tanesco) katika mabadiliko kuliangaza Taifa linalofanyika leo Jumatatu Julai 31, 2023 ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.