Makocha Watakaoanza na Presha Ligi Kuu Bara





BODI ya Ligi Kuu Bara (TPLB) imetoa kalenda yake ya msimu mzima wa 2023/2024 huku ikiweka wazi pazia la ligi litaanza rasmi Agosti 15 hadi Mei 25, mwakani.

Kabla ya kuanza kwa ligi hiyo inayokua kwa kasi kubwa ndani na nje ya nchi ila ilitatanguliwa na michezo ya nusu fainali ya Kombe la Ngao ya Jamii ambapo mabingwa watetezi Yanga itacheza na Azam huku Simba ikicheza na Singida Fountain Gate.

Wakati michezo hiyo itakayoanza kupigwa kuanzia Agosti 9, kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga ikisubiriwa kwa hamu ila kuna baadhi ya makocha watakaokuwa kwenye wakati mgumu msimu ujao na kama wasipokaza buti basi huenda wakafurushwa.

Licha ya ushiriki wa timu 16 kama ilivyokuwa msimu uliopita ila Mwanaspoti linakuletea baadhi ya makocha watakaokalia kaa la moto.


YOUSSOUPH DABO (AZAM FC)

Msimu huu Azam itakuwa chini ya Msenegali, Dabo aliyetambulishwa kuifundisha timu hiyo Mei mwaka huu baada ya kutokuwa na kocha mkuu tangu alipoondoka Mfaransa, Dennis Lavagne mwishoni mwa Oktoba mwaka jana kutokana na matokeo mabovu.

Tangu kuondoka kwa Lavagne, Azam ilikuwa chini ya kaimu kocha mkuu ikianza na Kali Ongala na baadaye Daniel Cadena, hadi mwisho wa msimu.

Dabo mwenye umri wa miaka 43, alikuwa kocha wa timu ya Tengueth FC ya Senegal iliyofuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2020/21 kwa kuwatoa wababe wa Morocco, Raja Casablanca kisha kutimkia klabu ya Jaraaf FC hadi mwaka jana.


Kocha huyo ana jukumu kubwa la kuiongoza timu hiyo kufikia nchi ya ahadi wakati huo itakaposhiriki michuano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ikiwemo Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

MIGUEL GAMONDI (YANGA)

Yanga ilimtambulisha rasmi Muagentina, Gamondi Juni 24 mwaka huu wakati wa mkutano mkuu wa klabu hiyo kuchukua mikoba ya Nasreddine Nabi aliyetua FAR Rabat ya Morocco.

Gamondi ambaye kwa mara ya kwanza kuiongoza timu kama kocha mkuu ilikuwa mwaka 1998 akiifundisha, Racing Club ya nchini kwao hadi 1999 anakabiliwa na kibarua kizito cha kutetea mataji yote ya ndani ambayo Yanga ilichukua kwa msimu ulioisha.

Mafanikio ya Nabi msimu uliopita akichukua Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la Afrika ndio yanayoleta maswali kwa Gamondi ni kwa jinsi gani ataweza kuitengeneza timu hiyo.


Gamondi mwenye miaka 56 anayetumia mfumo wa 4-2-3-1 atakutana na wakati mgumu wa kusuka mshambuliaji atakayevaa viatu vya mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika, Fiston Mayele anayeelezwa anatua Pyramids ya Misri.

ROBERTO OLIVEIRA 'ROBERTINHO' (SIMBA)

Robertinho ni miongoni mwa makocha watakaokuwa kwenye wakati mgumu msimu huu kutokana na matarajio makubwa ya viongozi na mashabiki zao baada ya kushuhudia kikosi hicho kwa misimu miwili mfululizo kikipokwa mataji na wapinzani wao Yanga.

Usajili wa Leandre Willy Onana, Luis Miquissone, Che Malone Fondoh, David Kameta 'Duchu' na Aubin Kramo ni ishara tosha ya jinsi gani Mbrazili huyo atakuwa kwenye presha kubwa msimu ujao wa kupambania mataji yote mbalimbali itakayoshiriki.

Robertinho aliyeteuliwa kuinoa timu hiyo Januari 3 mwaka huu akichukua nafasi ya Juma Mgunda aliyekuwa msaidizi wake, amekuwa na rekodi zuri kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara kwani tangu ateuliwe kipindi hicho hadi msimu unaisha hajapoteza.


Tangu Januari 3 hadi Juni 9 ambapo Ligi ilifikia tamati, Robertinho aliiongoza Simba katika michezo 11 ya Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hiyo alishinda tisa na kutoa sare miwili tu ambayo ni 1-1 dhidi ya Azam FC (Februari 21), 1-1 na Namungo (Mei 3).

HANS VAN DER PLUIJM (SINGIDA FOUNTAIN GATE)

Viongozi wa Singida Fountain Gate wameamua kumuongezea mkataba wa mwaka mmoja kocha mkuu wa timu hiyo, Pluijm hadi msimu ujao baada ya kumaliza nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kuipeleka katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Licha ya mafanikio hayo ila huu ni mtego kwa Pluijm kwani baadhi ya viongozi walikuwa wanataka kumtafutia mbadala wake jambo linaloonyesha dhahiri endapo hatokaza vizuri soksi zake basi huenda naye akapewa mkono wa kwaheri mapema sana.

MWINYI ZAHERA (COASTAL UNION)

Baada ya kuishusha Polisi Tanzania, Zahera msimu huu atakuwa na kikosi cha Coastal Union ambacho nacho msimu ulioisha chini ya Fikiri Elias, hakikuwa na wakati mzuri licha ya kunusurika pia na janga la kushuka daraja hadi Championship.


Zahera atakuwa na wakati mgumu wa kusuka timu hiyo ambayo imeondokewa na wimbi kubwa la wachezaji wakiwemo, Moubarack Amza, Gustapha Simon, Hamad Majimengi, Joseph Zziwa, Emery Nimubona, Mahamoud Mroivili, Djibril Naim Olatoundji na Juma Mahadhi.

Makocha wengine mbali na hao ni Denis Kitambi (Namungo FC), Abdihamid Moallin (KMC), Melis Medo (Dodoma Jiji) na Mecky Maxime wa Kagera Sugar.

KAULI ZA WADAU

Nyota wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa anasema msimu ujao utakuwa ni mgumu kwa kila timu hasa kutokana na ushindani uliopo.

"Msimu ujao unaonyesha wazi kila timu imejiandaa ndio maana unaona inajitahidi kufanya usajili mkubwa utakaoendana na mahitaji yao, kwangu naamini makocha wote watakuwa kwenye wakati mgumu hivyo tusishangae timua timua ikaanza mapema."

Kwa upande wa mchezaji wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua anasema msimu unaanza kutafsiriwa kutokana na maandalizi ya kila timu hivyo ukiangalia na kufanya tathimini ya sajili zilizofanyika hadi sasa unaona picha halisi ya ushindani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad