Mapya Yaibuka Afisa TRA Anayedaiwa Kujia Hotelini


Tanga. Familia ya Richard Walalaze, ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Arusha aliyedaiwa kujiua kwa kujirusha kutoka ghorofani, imesema haiamini kama kweli alijirusha.

Imeeleza inatia shaka tukio la kifo cha ndugu yao baada ya kuuona mwili wake katika chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Bombo na kufuatilia mahali ulipokutwa mwili huo hotelini.

Familia hiyo imeeleza kuwa imejikuta ikiwa na maswali mengi yasiyo na majibu, hivyo inasubiri taarifa ya uchunguzi wa mwili itakapotolewa na Serikali.

Msemaji wa familia hiyo, Mchungaji Godfrey Walalaze, ambaye ni kaka wa marehemu alisema hayo jana alipozungumza na Mwananchi, akiwa katika Hospitali ya Bombo.

Alisema mazingira ya kifo cha ndugu yao yanatia shaka iwapo ni kweli alijirusha kutoka ghorofani au la.

"Tumeuchunguza mwili tunapata shaka, sababu ukiacha kovu kichwani, mwili wote hauna mchubuko wala hakuna kiungo chochote kilichovunjika, lakini hata pale hotelini ulipokutwa mwili na michirizi ya damu inatupa maswali mengi mno," alisema Walalaze, ambaye ni mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Alisema mipango ya mazishi itategemea taarifa za Serikali kuhusu uchunguzi utakapokamilika.

"Tunawaza kufanya mazishi Jumatatu, Mlalo wilayani Lushoto, lakini itategemea na taarifa za Serikali kuhusu uchunguzi wa kifo cha mdogo wangu," alisema Walalaze.

Tukio lake


Habari zilizopatikana juzi na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Henry Mwaibambe, mtumishi huyo alijirusha kutoka ghorofa ya pili ya hoteli ya Ocean Breez jijini hapa usiku wa kuamkia juzi na inaelezwa alikuwa amepanga chumba katika hoteli hiyo tangu Julai 16, mwaka huu.

Mfanyakazi wa hoteli hiyo aliyeomba kuhifadhiwa jina lake, alisema Richard alipanga chumba namba 124 kilichopo ghorofa ya pili kilichokuwa jirani na cha mtumishi mwenzake wa TRA.

Alisema walimtilia shaka Richard kwa kuwa tangu jioni alisikika akizungumza kwa sauti kubwa akiwa chumbani kwake akisema anaogopa.


Alidai mwili wa Richard ulikutwa asubuhi na mfanyakazi aliyekuwa akifanya usafi hotelini hapo ukiwa chini usawa wa dirisha la chumba chake, jambo lililoashiria kuwa alijirusha.

“Tulikuta mwili ukiwa na kovu kichwani na damu nyingi. Alikuwa amevaa fulana na jeans. Mlinzi hakueleza kama alisikia kishindo au la…hata sisi hatuelewi nini kilimtokea,” alisema mtumishi huyo.

Alidai tangu alipowasili hotelini hapo alikuwa akisikitika kwamba hana raha, kwa sababu siku chache zilizopita alifiwa na baba yake mzazi na mkewe ambaye ni mjamzito yupo chumba cha wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU).

Hata hivyo, Mchungaji Walalaze alisema mdogo wake hakuwa ameoa wala hakuwahi kuwatambulisha kama ana mchumba.

Kamanda Mwaibambe hakupatikana jana kuzungumzia uchunguzi unaoendelea. Hata hivyo, juzi aliahidi kutoa taarifa utakapokuwa umekamilika.

Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Thomas Masese akizungumza na Mwananchi juzi alisema Richard alikuwa miongoni mwa maofisa wa mamlaka hiyo waliokuwa jijini Tanga kwa kazi maalumu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad