Mayele amshauri Fei toto, awatuliza mashabiki




Mshambualiji hatari wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Mkongomani Fiston Mayele amesema kuwa Jumatatu (Julai 10) itajulikana hatima yake ya kubaki ama kuondoka klabuni hapo mara baada ya kufanya kikao cha mwisho na uongozi wa timu hiyo, huku akimpa onyo swahiba wake, Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tangu, Fei Toto atambulishwe na Azam ilyompa mkataba wa miaka miwili ya kuichezea timu hiyo, kwa dau la Sh 200Mil.

Fei Toto ambaye ni rafiki wa karibu wa Mayele, tayari amejiunga na kambi ya Azam FC baada ya juzi kufanyiwa vipimo vya afya tayari kwa safari ya kambi ya nchini Tunisia.

Mayele amesema: “Hatima yangu ya kubakia au kuondoka Young Africans, itajulikana rasmi Jumatatu ijayo baada ya kukutana na uongozi na kufanya kikao cha mwisho, ninaamini tutafikia muafaka mzuri wa kubakia hapa.


“Mimi nipo tayari kubakia hapa, kwani Wakongo wengi wanapenda hela, na mimi nimekuja hapa nchini kutafuta hela sio kitu kingine, kama ikitokea tukashindwana basi ana basi  nitaondoka kwa amani kabisa bila ya kuwepo maneno maneno,” amesema Mayele.

Kuhusiana na Fei Toto kutua Azam FC, Mayele amesema kuwa Azam FC ni kati ya timu kubwa za kuogopwa kutokana na usajili ambao wanaoufanya katika kila msimu, lakini wanakosa makombe.

Ameongeza kuwa hilo tayari amemwambia Fei Toto, kwa kumtaka yeye awabadilishe na badala yake wacheze michezo yote katika kiwango bora bila ya kuangalia ukubwa wa timu wanayokwenda kukutana nayo.

“Juzi nilimwambia Fei Toto kuwa umekwenda kulekule ambako wenyewe wanakamia timu kubwa pekee za Simba SC na Young Africans, lakini wanapokutana na timu ndogo wanapoteza.

“Azam FC ni timu bora yenye wachezaji wengi wakubwa ambao kwenye mechi kubwa wanacheza vizuri tena kwa kukamia, lakini wanapocheza na timu ndogo wanacheza katika viwango vidogo,” amesema Mayele.

Usiku wa kuamkia jana Alhamis (Julai 06) , Mayele alikuwa sehemu ya watu waliotangaza uzi mpya wa Yanga ambao rasmi ulizinduliwa huko nchini Malawi na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera sambamba na Rais wa Young Africans, Injinia Hersi Said.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad