Luis Jose Miquissone |
Mchezaji Luis Miquissone Kurudi Simba SC Baada ya Kushindwa Al Ahly
Uongozi wa Simba SC upo katika mipango ya kumrudisha Kiungo Mshambuliaji Luis Jose Miquissone ambaye ameshindwa kufanya vyema ndani ya Klabu ya Al Ahly ya Misri ambao walimnunua kutoka Msimbazi.
Luis ambaye alijiunga na Al Ahly Agosti mwaka 2021 na kusaini mkataba wa miaka minne kwa sasa anafanya mazoezi binafsi huku mwenyewe akiweka wazi kuwa tayari kutafuta changamoto katika timu nyingine ili apate nafasi ya kucheza mara kwa mara ambayo kwa sasa haipati.
Chanzo cha ndani kutoka Simba SC kimesema kuwa kumekuwa na mazungumzo ya klabu hiyo kumrudisha Luis kutoka Al Ahly kwa mkopo ili kwenda kuwatumikia Msimbazi yameendelea vizuri na mchezaji mwenyewe anaonekana kuridhia.
“Simba SC ni kweli wapo katika mipango ya kumsajili Luis na ambacho kinafanyika kwa sasa ni mpango wao wa kumchukua kwa mkopo kisha wakubaliane namna gani watalipana haswa katika mshahara na mambo mengine.
“Kwa upande wa mchezaji ni wazi kuwa yupo tayari kuondoka na tayari uongozi unaomsimamia mchezaji umetuambia kuwa mchezaji anataka kupata timu nyingine ambayo itampa nafasi nzuri ya kucheza na sio kukaa nje kama sasa,” kimesema chanzo hicho.
Kwa upande wa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amefunguka kuhusiana na usajili huo akisema: “Simba kuna mchezaji tumemsajili ambaye kila timu watahofia kucheza na Simba, ni usajili ambao kila Mwanasimba ataufurahia hivyo siku ikifika wataelewa nini nilikuwa nasema.”