Mkazi wa Tabata, Gerald Mwangoka (24) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam akikabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa gramu 963.57.
Mshtakiwa huyo amefikishwa mahakamani hapo, leo Julai 21, 2023 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 36/2023, mbele ye Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate.
Hata hivyo, kabla ya kusomewa shtaka hilo, Hakimu Kabate alieleza mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali kutoka kwa Mwendesha Mashtaka ya nchini (DPP).
Hakimu Kabate baada ya kueleza hayo, upande wa mashtaka ulimsomea shtaka lake.
Akimsomea shtaka lake, wakili wa Serikali Eva Kassa, amedia mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 25, 2023 eneo la May Fair lililopo Mikocheni wilaya ya Kinondoni.
Inadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria, mshtakiwa alikutwa akisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa gramu 963.57.
Kwa mujibu wa wakili Kassa, amedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo, ameomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Kabate ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 3, 2023 itakapotajwa.
Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka linalomkabili, halina dhamana kwa mujibu wa sheria.