Mkurugenzi Amvua Madaraka Mganga Mfawidhi Hospitali ya Kivule




Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Jomari Satura, amemvua madaraka Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Kivule kwa kushindwa kusimamia majukumu yake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Julai 8, 2023 na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano, Tabu Shaibu, hatua hiyo imefikiwa baada ya kushindwa kuhakikisha utoaji wa huduma za afya katika kituo hicho unazingatia ubora, miongozo, taratibu na sheria za afya.
Taarifa hiyo inaeleza kwamba Satura ameelekeza muuguzi kiongozi wa wodi ya wazazi kuondolewa kwenye nafasi yake na kupangiwa majukumu mengine.

Hatua hizo zinakuja baada ya kusambaa kwa video iliyomuonyesha mtumishi wa hospitali hiyo akisafisha na kuanika juani vifaatiba nje ya jengo la hospitali, kitendo ambacho hakikubaliki kwa kuwa ni kinyume na taratibu na miongozo ya afya.

Kwa niaba ya uongozi wa jiji, Satura ameomba radhi kwa mamlaka na umma wote wa Watanzania kwa kitendo hicho kilicholeta usumbufu na taharuki.
Satura amemuagiza Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam kuhakikisha anasimamia kwa karibu utoaji wa huduma bora katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vya Serikali na binafsi.


“Ofisi ya Mkurugenzi inakemea vikali vitendo kama hivi na itahakikisha havijirudi tena na kuwataka watumishi wote wa sekta ya afya na sekta nyingine kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia miongozo na taratibu zote,” ameeleza Tabu kupitia taarifa hiyo.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad