Bukoba. Moto ambao chanzo chake hakijajulikana umeteketeza bweni la wavulana katika shule ya sekondari ya Istiqama iliyoko Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Hakuna majeruhi wala kifo katika tukio hilo la moto lililokea Saa 12:00 jioni ya Julai 7, 2023 wakati wanafunzi wakiwa katika uwanja wa michezo.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kagera, Zablon Muhumha amesema Askari wa jeshi hilo kwa kushirikiana na raia wema walifanikiwa kuudhibiti moto huo kabla haujasambaa kwenye majengo mengine.
"Askari wetu walifanikiwa kufika kwa wakati mara baada ya kupokea taarifa na kufanikiwa kuudhibiti moto huo wakishirikiana na wenzao wa kikosi cha Zimamoto cha uwanja wa ndege Bukoba," amesema Kamanda Muhumha
Amesema uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha moto huo na hasara iliyotokana na janga hilo.
Mkurugenzi wa shule ya sekondari Istigama, Farid Said amesema mali na vifaa vyote vilivyokuwa ndani ya bweni hilo lililokuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 70 imeteketea.
"Tunamshukuru Mungu hakuna madhara kwa binadamu. Tunawapongeza Zimamoto kwa kufanikiwa kuudhibiti moto usienee kwenye majengo mengine na kuleta madhara makubwa," amesema Said