Imeelezwa kuwa kiungo mshambuliaji wa Al Ahly ya Misri, Luis Miquissone raia wa Msumbuji ameletwa nchini kimyakimya na mabosi wa Simba na kufichwa katika mmoja ya hoteli maarufu zinazotumiwa na timu hiyo kufikia wachezaji wake.
Simba imekuwa ikihaha kumrudisha nyota huyo aliyejiunga na Mabingwa wa Afrika, Al-Ahly mwaka 2021 akitokea Simba lakini hakuweza kupenya na kuwa mchezaji muhimu ndani ya kikosi hicho kabla ya kutolewa kwa mkopo kwenye klabu ya Abha ya nchini Saud Arabia ambayo tayari amemaliza mkopo wake na kurejea kwenye timu yake.
Hata hivyo Miquissone mwenye uwezo wa kucheza nafasi zote tatu za mbele, amekuwa kwenye wakati mgumu kutokana na kutokuwa kwenye nafasi ndani ya kikosi hicho kwa msimu ujao hali inayomfanya kusaka timu mpya huku akitoa sharti maalum la kuweza kulipwa mshahara wa Shilingi million 80 ambazo analipwa kwa sasa na timu yake.
Taarifa za uhakika kutoka chanzo makini ndani ya klabu hiyo, uongozi wa Simba umelipitisha jina la Miquissone kuwa usajili wao mkubwa msimu ujao ambapo awali walimtaka wapewe kwa mkopo ambao utakuwa na makubaliano maalum na Al-Ahly katika kuweza kulipa mshahara wake.
“Miquissone yupo tayari na amekuwa katika hoteli ya Crown ambayo wachezaji wote wa Simba kutoka nje wamekuwa wakifikia na hayupo peke yake kwa sababu wapo wengine ambao hawajaenda Uturuki bado kutokana na uongozi kushughulikia mambo yao ya safari.
“Wakati wowote wanaweza wakatamtangaza kama mchezaji mpya wa Simba kutokana na mipango mengine kuendelea kwenda vizuri upande wa uongozi wa Simba na Al-Ahly juu ya Miquissone, unajua hakuna kitu ambacho kinawapa wakati mgumu uongozi kama lawama wanazopata kutoka kwa mashabiki ndiyo maana wamekuwa siriasi sana,” alisema mtoa taarifa.
Championi lilivyomtafuta Meneja wa Mawasiliano ya Simba, Ahmed Ally alisema kuwa kwa sasa wachezaji watatu ambao ambao bado hawajatambulisha huku mmoja kati yao utambulisho kuwa utatingisha nchini kutokana na ukubwa wake.
“Nadhani kwamba hatujamaliza wapo ambao tutaendelea kuwatambulisha na kuna mchezaji mmoja mkubwa sana ambaye utambulisho wake nchi itaenda kutikisika,” alisema Ahmed.