Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) wazalishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen, MwanaSpoti na mitandao mbalimbali ya kijamii wamelaani tukio la waandishi na dereva wo kushambuliwa wakati wakitekeleza majukumu yao
Dar es Salaam. Uongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya waandishi wawili na dereva wa MCL kushambuliwa wakitekeleza majukumu yao katika viwanja vya Bulyaga, Temeke, jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea mchana wa jana Jumamosi, Julai 22, 2023 wakati waandishi na dereva walipofika kufuatilia maandalizi ya mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chadema unaotarajia kufanyika leo Jumapili.
Mbali na kujeruhiwa kwa waandishi hao na dereva, pia wameibiwa simu za mkononi pamoja na gari kuharibiwa kwa kuvunjwa vioo.
Tayari uongozi umeripoti tukio hilo Kituo cha Polisi cha Chang’ombe kama hatua ya awali wakati taratibu zingine za kiofisi zikiendelea.
Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Ltd (MCL), Victor Mushi amesema shambulio hilo dhidi ya waandishi wake waliokuwa wakiripoti maandalizi ya mkutano wa hadhara, linahatarisha ustawi wa tasnia ya habari kwa kutengeneza mazingira yanayozuia wanahabari kufanya kazi zao kwa weledi.
Hivyo kuwanyima Watanzania fursa ya kupata habari na taarifa zinazowawezesha kufanya uamuzi katika dhima ya MCL ya kuwezesha taifa.
"Shambulizi hili la kusikitisha linakinzana na falsafa ya R4 ya Serikali ya Awamu ya Sita inayozungumzia Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya kama msingi wa siasa za kidemokrasia Tanzania," amesema Mushi
"Watanzania wana haki ya msingi ya kuhabarishwa, na sisi kama chombo cha habari tunapaswa kuweze kufanya kazi zetu bila bughudha ili tuwapatie habari kwa ukamilifu – bila hofu."
Mushi amesema, MCL inatarajia vyombo vya ulinzi na usalama vitimize wajibu wake kwa kuchunguza suala hili kwa undani na kuwachukulia hatua wale wote waliohusika katika kuwashambulia waandishi wake.