Mwenye Namba Yake Karudi, Unaambiwa Huko Simba Mambo ni Moto Kweli Kweli



HABARI ya mjini kwa sasa ni Simba kufanikiwa kumrejesha kikosini nyota wake wa zamani kutoka Msumbiji, Luis Miquisone ikimsajili kama mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba wake na vigogo wa Afrika, Al Ahly ya Misri.

Awali, Simba ilisajili Miquissone 2020 akitokea UD Songo ya Msumbiji na kudumu Msimbazi kwa misimu miwili kabla ya kumuuza Al Ahly, 2021.

Msimu mmoja Miquissone aliyokaa Simba ilikuwa bora kwake, katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa na kufanikiwa kufunga jumla ya mabao tisa na kutoa asisti 15.

Ubora aliokuwa nao ndio uliwafanya Al Ahly wavutiwe na kumsajili kwa pesa zaidi ya Sh 2 bilioni za Kibongo.

Hata hivyo maisha ya Miquissone ndani ya Al Ahly yalibadilika, hakupata nafasi ya kutosha kucheza kwenye mechi na baadae akatolewa kwa mkopo katika klabu ya Abha ya Saudi Arabia lakini hata huko mambo yalikuwa yale yale na baadae akarejea Al Ahly kabla ya kuamua kuvunja mkataba.

Pamoja na kushindwa kuonyesha makali huko Al Ahly na Abha sasa anarudi Simba wakati namba yake ikionekana kuwa bado ipo wazi kutokana na wachezaji wengi waliosajiliwa kuziba pengo lake kushindwa kufanya hivyo na hadi sasa Simba haijapata mchezaji mwingine kama Miquissone.

Mwaaspoti kupitia makala haya linakuletea baadhi ya wachezaji wa kigeni waliosajiliwa katika nyakati tofauti ili kuziba pengo lililoachwa na Miquissone upande wa winga Simba lakini wakashindwa kufanya hivyo na sasa anarejea mwenye namba yake.

PAPE SAKHO

Moja kwa moja baada ya kuondoka kwa Miquissone jicho la Simba lilitua nchini Senegal katika klabu ya Teungueth na kumsajili Pape Sakho anayetumia zaidi mguu wa kushoto.

Simba iliamini Sakho ataziba pengo la Miquissone lakini hakuweza kufanya hivyo licha ya kwamba kwa nafasi yake alionyesha ubora kiasi.

Sakho sasa huenda akaachana na Simba baada ya kupata dili jipya Ufaransa katika Ligi Daraja la Pili na anaondoka huku Pengo la Miquissone likionekana bado wazi.

Msimu uliopita Sakho aliifungia Simba mabao tisa kwenye ligi na kutoa asisti mbili.

PETER BANDA

Pia mwaka 2021 Simba ilisajili winga mwingine, Peter Banda kutokea Big Bullet ya kwao Malawi ikiwa ni muendelezo wa kutafuta mkali kama Miquissone.

Banda hajaziba pengo la Miquissone Simba na muda mwingi amekuwa mejeraha jambo lililomfanya kushindwa kuonyesha ubora wake mfululizo.

Banda naye licha ya kuwa kambini uturuko lakini msimu ujao anaweza asivae jezi ya Simba.

DUNCUN NYONI

Huyu naye alitua Simba wakati mmoja na Sakho na Banda akitokea Silver Strikers ya kwao Malawi lakini hakuthubutu hata kidogo kuonyesha kuziba pengo la Miquissone.

Uwezo wa nyoni haukuwashawishi mashabiki wa Simba hata kumfikiria kuziba pengo la Miquisone pia hakuwa anapata nafasi mara kwa mara kwenye kikosi cha Simba.

Nyoni alidumu Simba kwa kipindi cha nusu msimu na baada ya hapo alivunjiwa mkataba na kurejea kwao na hadi sasa anaichezea Silver Strikers.

BERNARD MORRISON

Huku na huku Simba ikadondoka Yanga na kumchomoa winga Machachari Bernard Morrison ikiamini atakuwa mbadala halisi wa Miquissone.

Morrison akaetua Simba na kuanza kucheza, ikawa tripu shamba, tripu geriji. alicheza mechi chache Simba lakini pia hakuwa tegemeo kwenye kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa kwa Miquissone.

Mwana 2022 Simba ikaona isiwe tabu, ikaachana na Morrison na winga huyo akarejea Yanga ambako nako ameachwa msimu uliopita.

AUGUSTINE OKRAH

Baada ya Sakho, Banda, Morisson na Nyoni kushindwa kuziba vyema pengo la Miquissone, Msimu huu Simba ikarudi Sokoni na kumsajili Augustine Okrah kutokea Bechem United ya kwao Ghana.

Okrah akaanza kazi Simba, mambo yakaanza kutoeleweka, vurugu zikawa nyingi, majeraha yakamuandama na misho wa siku msimu ukaisha akiwa hajafanya vyema ndani ya timu hiyo.

Simba ikashindwa kumvumilia na mwishoni mwa msimu uliopita ikaagana naye akiwa amefunga mabao manne tu kwenye ligi na sasa yupo kwao Ghana akisikilizia timu mpya.

Kiujumla Simba imehaha kupata mrithi wa Miquissone kwa kusajili lundo la wachezaji wengi wa kigeni lakini wapeshindwa kuziba na sasa imeamua kumrudisha mwenye namba yake.

Kama atakuwa bado kwenye kiwango bora kama kile alichoonyesha kabla hajaondoka Simba, Miquissone huenda akaingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha Simba licha ya kwamba wamesajiliwa wachezaji wengine wapya katika maeneo yake.

Pale Simba Miquissone msimu ujao atashindania namba na Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’, Kibu Denis, Willy Onana na Kramo Aubin.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad