Arusha. Serikali imesema ndege aina ya Airbus A220 ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) iliyokuwa ikishikiliwa nchini Uholanzi imeachiwa na kurejea nchini jana.
Hayo yamesemwa leo leo Julai 8, 2023 mjini hapa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alipozungumza na waandishi wa habari juu ya masuala mbalimbali ikiwamo utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
“Leo niko hapa kuwapa habari njema, siku chache zilizopita niliwajulisha kuna ndege yetu tulikuwa na kesi nchini Uholanzi ikakamatwa, ilikuwa chini ya mikono ya sheria. Bahati nzuri tumefanya mazungumzo na jambo limekwenda vizuri ndege yetu imerudi jana jioni iko Tanzania,” amesema Msigwa na kuongeza;
“Chuma kimerejea kiko Tanzania… inaendelea kuandaliwa ili ianze shughuli zake, tunaendelea kuimarisha shirika letu, mambo yetu yatakuwa yaanaendelea kuwa mazuri. Tunafahamu tumepokea ndege ya mizigo na habari njema jana imeanza safari zake za kusafirisha mizigo Dubai na unakwenda Marekani. Tuna ndege zetu nyingine tatu ambazo zitakuja mwishoni mwa mwaka huu na mapema mwakani.”
Kwa mujibu wa msemaji huyo, Serikali inaliangalia shirika hilo la ndege kama la kimkakati na kwamba ripoti ya CAG inaendele kuwaonyesha wanahitaji kufanya vizuri kwwa kuliboresha.
“Shirika letu la ndege lilikuwa limekufa kwa sasa tunalifufua na linaendelea kuboreshwa, tunataka tuwe na shirika la ndege lenye nguvu na kwa sasa linafanya kazi vizuri,” amesema.
Gazeti la Mwananchi, Desemba mosi, 2022 liliripoti taarifa ya Serikali ikiwatoa hofu Watanzania kuhusu kushikiliwa kwa ndege hiyo, ikisema haiwezi kutaifishwa kutokana na rufaa ya kesi iliyokuwa ikiendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID).
Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa wakati huo viliripoti kuhusu mwekezaji wa Sweden aliyeshinda tuzo ya Dola 165 milioni (Sh380 bilioni) dhidi ya Tanzania na kuishawishi Mahakama ya Uholanzi kushikilia ndege hiyo kama kigezo cha kushinikiza malipo yake, licha ya kutopata uhalali wa ICSID.
Akizungumzia suala hilo kwa wakati huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi alikiri mwekezaji huyo kushinda tuzo hiyo na ndege imeshikiliwa hata hivyo aliwatoa hofu watanzania huku akisema Serikali iko makini katika jambo hilo.