JINA la Fiston Mayele halikuwepo katika orodha ya wachezaji waliotambulishwa Jumamosi jioni wakati Yanga walipofanya tamasha lao la wiki ya Mwananchi. Hakuna aliyeshangaa sana. Moja kati ya siri ambazo zimefichwa vibaya ni kwamba Mayele ameuzwa. Kila mtu anafahamu.
Haikushangaza kuona jina lake halikuwepo. Yanga waliandaliwa kisaikolojia. Ingawa hadi jana ilikuwa haijatangazwa rasmi, lakini ilishavuja kwamba Yanga wamemuuza Mayele kwenda Misri kwa zaidi ya dola 1.2 milioni.
Kilichowashangaza baadhi ya mashabiki ni kukosekana kwa Wakongo wenzake wawili, Djuma Shaabani na Yannick Bangala. Kwanini hawakuwepo? Inamaanisha kwamba hawatakuwa wachezaji wa Yanga kuanzia msimu huu unaoanza siku chache zijazo.
Vyanzo vyangu vya ndani vinaniambia kwamba Djuma na Bangala wameachwa kwa sababu ya kuongoza migomo ya mara kwa mara. Lakini kuna taarifa za kiitelejensia kinaonyesha kwamba hawakuwa ‘wenzao’ katika baadhi ya mechi muhimu.
Baadaye waliomba kuondoka klabuni. Hata hivyo ni kama walikuwa wanatishia tu. Mabosi wa Yanga walipoamua kuwakubalia kuondoka klabuni hapo walipigwa na butwaa. Wakaomba radhi na kutaka kuendelea kubakia lakini walikuwa wamechelewa.
Hawakuwa wamesoma alama za nyakati. Kuna wachezaji ambao wanweza kutishia kuondoka klabu na klabu pamoja na nchi nzima ikatisikika. Ni kama ambavyo Clatous Chotta Chama alipotingisha wakati iliposemekana kwamba anataka kuondoka Simba siku kadhaa zilizopita.
Alikuwa mchezaji sahihi kutingisha. Kwa Djuma na Bangala imekuwa hadithi tofauti. Nadhani hawakusoma alama za nyakati. Wakati wanatishia kuondoka hawakusoma vema umuhimu wao katika klabu ya Yanga.
Yanga wamekuwa na msimu mzuri. Wamefika katika fainali za Shirikisho wakiwa na timu nzuri. Wamechukua ubingwa wa Bara na ule wa FA wakiwa na timu nzuri. Hata hivyo ulikuwa ni msimu ambao Djuma na Bangala walionekana kuwa wachezaji wa kawaida.
Kwa Djuma tangu amefika nchini mashabiki wa Yanga wamesubiri kwa muda mrefu kumuona yule Djuma ambaye alitamba na klabu ya AS Vita. Ni Djuma ambaye mashabiki wa Yanga hawakuamini kama wangeweza kumnasa.
Mashabiki na viongozi wa watani wao nao hawakuamini kama Yanga walikuwa wamefanikiwa kuinasa saini ya staa huyu. Ilionekana ni sehemu ya mapinduzi makubwa katika Yanga. Ilionekana pia ingekuwa mwisho wa kijana wa Morogoro, Shomari Kibwana ambaye naye anacheza nafasi ya ulinzi wa kulia.
Hata hivyo Djuma hakuwa yule. Licha ya kuonekana kuwa na akili nzuri akiwa amelikaribia lango la wapinzani kwa sababu hapendelei kubutua bila ya kujua wapi anakoipeleka krosi yake lakini Djuma alionekana kukosa wepesi.
Baadaye aliandamwa na unene. Labda kwa sababu aliona mpira wa Tanzania ni mwepesi. Hakujibidiisha sana. Hata hivyo hilo lilimpa unafuu Kibwana kwa sababu alionekana kuwa bora zaidi katika ukabaji kuliko Djuma.
Mwisho wa kila kitu kwa miaka miwili ambayo ameishi nchini, Djuma hakuwahi kufikia ubora wake wa Vita. Hilo liliwanyima raha mashabiki wa Yanga ambao wangependa kuona Djuma anamfunika mlinzi wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe ambaye kwa muda mrefu amekuwa mlinzi bora zaidi wa kulia nchini.
Wakati akiongoza migomo klabuni, au wakati alipoomba kuondoka, Djuma angepaswa kupima ubora au umuhimu wake klabuni. Kama angekuwa katika kiwango kile kile alichokuwa nacho Vita basi si ajabu angekuwa mchezaji muhimu klabuni kama ilivyo kwa Mayele na wengineo.
Kama angekuwa katika kiwango cha Vita nadhani Yanga wangehaha vilivyo kumbakisha. Lakini pia kama angekuwa katika kiwango kile kile alichokuwa nacho vita basi Simba na Azam zingekimbizana vilivyo kusaka saini yake. Hakusoma alama za nyakati.
Halafu kuna Bangala. Msimu wake wa kwanza alikuwa bora wa Ligi Kuu nchini. Hakuna aliyebisha. Ni nadra kumpa mchezaji bora katika Ligi huku akicheza nafasi ya kiungo wa chini. Ni katika msimu ambao Chama alikuwa Morocco na viungo wengi wa mbele hawakufanya maajabu.
Wote tukakubali kwamba Bangala alistahili. Alihaha uwanjani. Alikuwa kila sehemu. Uwezo wake wa kumiliki mpira. Uwezo wake wa kupandisha timu, uwezo wake wa kukaba. Alikuwa kiongozi haswa uwanjani.
Binafsi nilimfananisha na staa wa zamani wa Simba na Yanga, Method Mogella. Linapokuja suala la kiungo wa chini kuwa mwanasoka bora wa msimu nadhani mchezaji wa mwisho kushinda tuzo hiyo alikuwa Marehemu Issa Athuman wa Yanga miaka mingi iliyopita.
Wakati George Mpole na Mayele wakiwania kiatu cha dhahabu, Bangala aliwakosha wengi baada ya kutajwa kuwa mchezaji bora wa msimu. Tatizo lilikuja msimu ulioisha. Ghafla aligeuka kuwa mchezaji wa kawaida.
Hakuwa Bangala yule ambaye tulimfahamu. Kuna mechi kadhaa muhimu za Yanga akaishia kukaa benchi. Wakati hali ikiwa hivyo kwake, pacha wake wa uwanjani, Khalid Aucho akaibuka kuwa mchezaji muhimu zaidi uwanjani kuliko yeye.
Wakati akiwa anapambana katika suala la usumbufu dhidi ya mabosi wake nadhani nakupima sana umuhimu wake klabuni. Wakati akiandika barua ya kuomba kuondoka hakupima sana umuhimu wake klabuni. Kama ingekuwa Aucho nadhani Yanga ingetikisika kidogo.
Bangala wa msimu wa kwanza Yanga wasingethubutu kumringia. Bangala wa msimu wa kwanza angetakiwa kwenda Simba na Azam kwa dau kubwa la mshahara. Sidhani kama timu hizi zina mpango huo. Naona zishakamilika kuchukua wachezaji wanaowataka. Kwanini wasimchukue Bangala bure?
Hivi ndivyo ambavyo Bangala na Djuma walishindwa kusoma alama za nyakati. Unahitaji kuwa mchezaji muhimu kama Chama kuweza kuzitikisa Simba na Yanga. Unahitaji kuwa Djidui Diarra, au Mohamed Hussein Tshabalala, au Shomari Kapombe, au Dickson Job, au Joyce Lomalisa na wachache wengineo.
Yanga wamefanya vizuri katika msimu ulioisha lakini siri kubwa ni kwamba wamecheza kitimu zaidi. Hawakutegemea sana uwezo wa mchezaji mmoja na ndio maana walifika mbali. Haikushangaza kwamba hata Fei Toto alipoamua kuondoka bado waliendelea kuwa imara katika michuano yote waliyoshiriki.
Pengo kati ya wanaonza na wanaokaa benchi sio kubwa. Akina Djuma wangesoma alama za nyakati kwa kuongeza umuhimu zaidi juu ya wenzao nadhani Yanga wasingechukua maamuzi haya. Wasingepata jeuri hii ambayo wameipata. Haishangazi kuona hata maamuzi yao hayajalaumiwa sana na mashabiki walio wengi. Mwingine ambaye inabidi ajitazame zaidi ni Stephane Aziz Ki. Na yeye hajafikia matarajio kwa kiasi kikubwa.