Kenya. Wafuasi wa Kiongozi wa upinzani nchini humo, Raila Odinga wamejikuta katika wakati mgumu baada ya maandamano yao kupigwa mabomu ya machozi huku baadhi yao wakikamatwa na polisi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Polisi huko Nyahururu walimkamata aliyekuwa Gavana wa Laikipia, Ndiritu Muriithi na mwanasiasa wa Jubilee Carolyne Mwendia kwa madai ya kushiriki maandamano haramu.
Mapema asubuhi ya leo Julai 7, 2023 baadhi ya waandamanaji waliifunga barabara kuu ya Thika na kufanya isipitike kwa kuziba sehemu za barabara katika hoteli moja ya Kitalii kwa kuwasha moto ambapo baadaye waandamanaji walitawanywa na barabara ikasafishwa.
Mjini Mombasa, polisi walirusha vitoa machozi kuwatawanya mamia ya wafuasi wa upinzani walioandaa maandamano katika barabara ya Moi Avenue.
Seneta wa Mombasa, Mohammed Faki, Mwakilishi wa Wanawake, Zamzam Mohammed na Mbunge wa Mvita Machele Mohammed waliongoza waandamanaji kuandamana hadi katikati mwa jiji.
Katika mtaa wa Kimathi jijini Nairobi, kundi la waandamanaji walilazimika kukimbia ili kujilinda baada ya maofisa wa polisi kuwarushia vitoa machozi.
Hata vivyo sehemu nyingi za Nairobi, zilibaki tulivu huku wenyeji wakiendelea na biashara zao kama kawaida.
Akiwa Kamukunji, Odinga aliwaongoza wafuasi wake katika kuwakumbuka wote waliopigania mfumo wa vyama vingi nchini humo akiwataja Kenneth Matiba, Joseph Murumbi, Jaramogi Oginga Odinga na yeye mwenyewe.
"Leo haitakuwa kama siku nyingine. Tuliwaambia wakome kuingilia vyama vyetu. Sasa, wabunge 25 wa Jubilee na saba kutoka ODM wamepelekwa UDA," alisema.
Msako mkubwa wa polisi umeshuhudiwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Homa Bay, ambapo barabara ya Rongo ilikuwa imefungwa na vijana ambao waliwasha moto.
Huko Shinyalu, Kakamega, maofisa wa polisi walipambana na waandamanaji na kulazimika kurusha vitoa machozi ili kuwatawanya.
Wengi wa vijana wanaoandamana ni wanatajwa kuwa ni waendesha boda boda ambao wameathiriwa sana na kupanda kwa bei ya mafuta, ambayo imetajwa na upinzani kuwa msingi wa maandamano ya leo.
Kwingineko huko Siaya, biashara zilisalia zilifungwa tangu asubuhi huku wenyeji wakiendelea kujitokeza mjini kujiunga na maandamano ya kuipinga serikali.
Shughuli katika Mji wa Kisii zilisimama tangu mapema asubuhi baada ya waandamanaji kufunga barabara kadhaa ndani ya mji huo.
Maofisa wa polisi waliotumwa waliripotiwa kurejesha hali ya usalama katika mji huo huku kukiwa na taarifa kwamba maofisa wengi kutoka eneo hilo walitumwa Kisumu, ambayo inachukuliwa kuwa sehemu kuu ya maandamano.
Inasemekana Odinga aliwaagiza baadhi ya wabunge wake kuongoza maandamano katika maeneo yao.
“Tuko hapa kutangaza kwamba mkutano wetu wa Kamukunji uko Nairobi Ijumaa hii, kama tulivyotangaza. Lakini si Kamukunji tu jijini Nairobi, bali ni Kamukunji kote nchini ambapo Ukombozi huu wa Tatu utazinduliwa,” Odinga alisema wakati wa kikao na wanahabari majuzi.
Odinga alisema leo Julai 7, 2023, watazindua zoezi la kukusanya saini (Petition) kupinga utawala wa Kenya Kwanza na sera zake, haswa ushuru.