Chanzo cha ndani kutoka ndani ya Simba kinasema kuwa, nyota hao wawili waliokuwa miongoni mwa wachezaji waliokiwasha msimu uliopita, wameshamalizana na mabosi wa timu hiyo kwa vile wana mikataba na msimu ujao watakuwa sehemu ya kikosi cha Singida iliyo mbioni kufahamika kama Singida Fountain Gate baada ya kuunganisha klabu hiyo na ile ya Fountain Gate ya Dodoma.
Onyango ni kati ya wachezaji waliokuwa wakiomba kuondoka Msimbazi tangu dirisha dogo la msimu uliopita kabla ya kuongezwa mkataba wa mwaka mmoja na inaelezwa aliandika tena barua kukumbushia ombi lake la kuruhusiwa kusepa, akiwamo winga Mmalawi, Peter Banda.
Kyombo aliyesajiliwa msimu uliopita akitokea Singida iliyomsajili awali kutoka Mbeya Kwanza iliyoshuka daraja kabla ya Simba kuomba iachiwe iwe naye baada ya wao nao kumsainisha mkataba na klabu hizo mbili zikakubaliana kunusuru kipaji ya nyota huyo wa zamani wa Mbao FC aliyewahi kusajiliwa na Mamalodi Sundowns ya Afrika Kusini.
"Kila kitu kimekaa sawa, muda wowote Kyombo na Onyango watapewa mkono wa kwaheri, kwani wameshamalizana na viongozi wa Simba na wataenda Singida inayowahitaji," kilisema chanzo hicho makini kilchoomba kuhifadhiwa jina.
Kyombo ni mmoja ya wachezaji waliofanyiwa vipimo vya afya wa klabu ya Simba mapema wiki hii ikiwa ni maandalizi ya timu hiyo kwenda kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya (pre season) itakayofanyikia Uturuki kwa muda wa wiki tatu.
Timu hiyo ya Simba inatarajiwa kuondoka Jumanne ijayo, mara baada ya kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' kuwasili nchini kuanzia usiku huu wa Alhamisi kuungana na wachezaji waliosalia kutoka kikosi cha msimu uliopita na wapya walioanza kutambulishwa akiwamo Leandre Onana.
Kutemwa kwa wachezaji huo kutaifanya Simba kufikisha idadi ya nyota 11 waliopewa 'Thank You' wakiwamo Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Kipa Beno Kakolanya, Victor Akpan, Nelson Okwa, Augustine Okrah, Ismael Sawadogo na Mohamed Ouattara.