ONYO! Wafanyakazi wa ndani wasiitwe 'Dada'



Watu ambao wameajiri wafanyakazi wa ndani wanawake wameonywa wasiwaite wafanyakazi hao jina la dada kwani inadaiwa kuchangia kunyima haki zao.


Sambamba na hilo pia wameonywa kutowaita majina ambayo yanadhalilisha utu wao ikiwemo 'beki tatu'. Onyo hilo limetolewa na Mwanasheria wa Chama cha wafanyakazi wa Majumbani, hifadhi ,hotelini, huduma za jamii na ushauri (Chodawu), Wagala Shungu, katika mafunzo ya kuwajengea uwelewa waandishi kuhusu mkataba namba 189 unaoeleza stahiki wanazopaswa kupewa wafanyakazi hao.


Shungu ambaye pia ni Katibu wa chama hicho, amesema wanapaswa kuwaita ‘mfanyakazi wa nyumbani’ kwasababu neno dada linamfanya mwajiri wake kuleta mahusiano ya kindungu badala ya ajira wakati uhusiano wao upo kwenye ufanyakazi.


Shungu amesema kitendo cha kumuita mfanyakazi huyo dada kinajenga ukaribu na hivyo pale anapotaka kudai haki zake ikiwemo mshahara bosi anamchukulia kama ndugu na kujipangia muda wa kumlipa.


"Mfanyakazi akitaka mshahara wake utaanza kumpa maneno matamu unajua mdogo wangu sijapata nitakupa siku fulani na kwa kuwa alishajenga udada na wewe inabidi tu akubali kwa kuwa tayari kashajiona ni sehemu ya familia,"amesema Mwanasheria huyo.


Akizungumzia kuhusu mkataba namba 189, amesema mkataba huo ulipitishwa nchini Geniva mwaka 2011, ambao unajulikana kama 'mkataba wa wafanyakazi wa majumbani' ambao mpaka sasa Tanzania bado haujauridhia.


Shungu amesema pamoja na mambo mengine mkataba huo unaeleza haki mbalimbali wanazopaswa kupewa wafanyakazi hao, ikiwemo kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na haki ya faragha ambayo hayapo kwa sasa katika sheria za kazi za nchi.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wafanyakazi majumbani, Zanini Othuman, amesema kupitia mkataba huo na elimu ambayo ameipata ameona namna gani mfanyakazi wa ndani anavyotakiwa kuthaminiwa kama wafanyakazi wengine ikiwemo likizo ya ujauzito.


Mkuu wa Idara ya Sheria ya Chadowu, amesema mafunzo hayo kwa waandishi wanaamini yataweza kusaidia kufikisha elimu mbali nini kilichopo ndani ya mkataba huu na kwa nini wanaupigania kuridhiwa.


Pia amesema wanahitaji kuondoa upotoshaji kuhusiana na mkataba huo ikiwemo tafsiri mbaya iliyotolewa juu ya umuhumu wa mfanyakazi kuwa na faragha.


"Kumekuwa na upotoshaji kuwa fargha inayotakiwa kwa mfanyakazi wa majumbani katika mkataba huo ni kuja na mme wake, jambo ambalo sio kweli bali ni kuwa na chumba chake ambacho kina mahitaji yote na kwa kufanya hivyo hakutamsaidia yeye tu bali na watoto wa mwajiri kwani kwa kulala nao inaweza kuleta sintofahamu kama ambavyo matukio mbalimbali yamekuwa yakiripotiwa ikiwemo ukatili wa kingono,"amesema

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad