UPO uwezekano mkubwa wa Simba kuendelea na kocha wake msaidizi, Juma Mgunda katika msimu ujao licha ya usiri mkubwa ulikuwepo kati yake na mabosi wa timu hiyo.
Mgunda juzi aliachwa katika msafara wa timu hiyo, uliosafiri kwenda nchini Uturuki kwa ajili ya kambi ya wiki tatu kujiandaa na msimu ujao.
Mgunda ni kati ya makocha waliounda benchi la ufundi la Simba lililoifikisha timu hiyo Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita akiwa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ raia wa Brazil.
Ikumbukwe kuwa, Simba juzi ilitambulisha benchi lao jipya la ufundi ambao ni kocha wa makipa Daniel Cadena, Meneja Mkuu wa Sayansi ya Michezo, Mikael Igendia na kocha viungo, Corneille Hategekimana.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Simba, kimesema kuwa, Mgunda huenda asiwe sehemu ya benchi la ufundi msimu ujao baada ya Robertinho kuomba aletewe msaidizi mwingine.
Kilisema kuwa, uongozi wa Simba hivi sasa unaangalia nafasi nyingine mpya ya kumpa kati ya hizo ni Kocha Mkuu wa Timu ya Wanawake, kama wakifikia muafaka mzuri.
Kiliongeza kuwa, Mgunda yeye bado hajaamua hatima yake ya kuchukua nafasi hiyo, lakini taarifa zilizopo kocha huyo anataka kurejea Coastal Union ya Tanga.
“Mgunda hatakuwa sehemu ya viongozi ya benchi la ufundi, kwani yapo mazungumzo yanayoendelea kati yake na uongozi wa Simba kujadiliana baadhi ya vitu kuelekea msimu ujao.
“Uongozi unahitaji kuendelea na Mgunda kwa nafasi nyingine katika timu, kati ya hizo kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Wanawake ya Simba.
“Lakini yeye anaonekana kutohitaji kuwa katika nafasi hiyo, bado mazungumzo yanaendelea kati yake na uongozi,” kilisema chanzo hicho.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alizungumzia hilo kwa kusema: “Mgunda hatokuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu wakati tutakapokuwepo Tunisia, kwani yeye amebaki kwa ajili ya kushughulikia mambo yake.”