Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francisco amemteua Askofu Mkuu Mwandamizi Jimbo Kuu la Tabora, Protase Rugambwa kuwa kardinali nchini Tanzania.
Rugambwa anakuwa kardinali wa tatu nchini Tanzania akitanguliwa na Laurean Rugambwa aliyefariki dunia Desemba 8, 1997 na Polycarp Pengo aliyestaafu mwaka 2019.
Papa amemteua Rugambwa kuwa kardinali ikiwa ni takribani miezi mitatu tangu alipomteua kuwa askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo Kuu la Tabora.
Askofu Rugambwa aliwahi kuwa askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma tangu mwaka 2008 hadi mwaka 2012 pamoja na Katibu Mkuu wa Idara ya Uinjilishaji Vatican.
Kwa mujibu wa tovuti ya Vatican Radio, Askofu Rugambwa alizaliwa Mei 31, 1960 mkoani Kagera na kabla ya kupata daraja la upadri alisoma katika seminari ndogo za Katoke, iliyoko Jimbo la Rulenge-Ngara na Itaga mkoani Tabora.
Taarifa za uteuzi huo, zimethibitishwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima akisema uteuzi huo ni, “ni baraka kwa Taifa letu,”.