Pape Ousmane Sakho wa SIMBA Huyooo, Anasepa zake Kibabe

 


Simba juzi ilimtambulisha Fabrice Ngoma aliyekuwa Al Hilal ya Sudan ili kukiongezea nguvu kikosi cha timu hiyo, huku winga machachari, Pape Ousmane Sakho inadaiwa ameomba kusepa klabuni hapo ili aenda kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.


Inaelezwa, Sakho amepata ofa kadhaa kutoka nchi za Ubelgiji na Ufaransa, lakini bado ana mkataba na Simba hivyo memejimenti ya mchezaji huyo imeuandikia uongozi wa Msimbazi kuomba imruhusu kuvunja mkataba ili adili na ofa alizonazo.


Sakho aliyesaliwa na mkataba wa mwaka mmoja na Simba inadaiwa ana ofa kutoka Stade Malherbe Caen na Grenoble zinazoshiriki Ligi Daraja la Pili Ufaransa, lakini ikielezwa kuna klabu nyingine ya Ubelgiji nayo inamtaka japo jina la timu halijafahamika.  


Sakho amepata ofa hizo baada ya mfululizo wa kiwango bora ikiwamo kuitwa timu ya taifa ya Senegal pamoja na tukio bora kwake ikiwemo ile Tuzo ya Bao Bora la michuano ya CAF msimu wa 2021/2022.


Mwanaspoti limejiridhisha jopo la wasimamizi wa Sakho limetuma ofa mezani kwa Simba likitaka wamuachie kiungo huyo akatafute maisha mapya, lakini hadi sasa hawajajibiwa kutokana na kile kinachodaiwa Simba inasikilizia dili la Miquissone litiki kwanza ndipo wamruhusu Sakho kuondoka.


Hata hivyo, upande wa Sakho umeendelea kusimamia msimamo wake wa kutaka staa huyo aondoke Simba na kutimkia Ufaransa wakiamini huko atavuna mkwanja mrefu na kupata maisha bora zaidi kisoka.


Hadi sasa Sakho anasikilizia uhamisho huo kukamalika na wakati Simba ikiwa Uturuki kwa maandalizi ya msimu ujao 'Pre Season', Sakho yeye yupo zake nchini kwao Senegal akiendelea kusubiri hatma yake.


Gazeti hili linajua kama Simba itashindwa kumuachia Sakho katika kipindi hiki, staa huyo atarejea kikosini, lakini hataongeza mkataba na atacheza hadi msimu umalizike kisha aondoke akiwa mchezaji huru.


Uongozi wa Simba ulipotafutww ili kupata ufafanuzi juu ya ofa hizo za Sakho, simu za viongozi ziliita bila kupokelewa kwa kilichoelezwa walikuwa kwenye kikao na hata Ofisa Habari wa timu hiyo, Ahmed Ally alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakuujibu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad