Mkurugenzi mkuu wa lebo ya Next Level Music, Rayvanny amejitokeza waziwazi na kukana kuwa na akaunti yoyote kwenye mtandao wa Facebook, licha ya kuwepo na akaunti yenye jina lake na amabyo imehakikiwa na kudhibitishwa na Facebook ikiwa na wafuasi Zaidi ya milioni 2.
Kupitia instastory yake, Rayvanny alipakia picha ya skrini ambapo ukurasa huo wa Facebook unaodhaniwa kuwa wake ulikuwa unajitangaza kwamba akaunti hiyo ilikuwa sokoni tayari kuuzwa kwa mnunuzi yeyote ambaye angeafikia bei.
“Nauza huu ukurasa kwa kampuni au hata msanii yoyote anayetaka kukua kimataifa, njoo DM lakini wanunuzi wenye wako serious pekee,” Ukurasa huo uliandika.
Mtu huyo ambaye awali alidhaniwa kuwa Rayvanny hadi alizidi kusema kwamba sababu ya kuipiga mnada akaunti hiyo ni kuwa anataka kusalia kwenye mitandao mingine tu kama Instagram na Tiktok katika kile alitaja kuwa hawezi kuzi manage zote.
Vannyboy aliweka wazi kwamba huyo ni mtapeli anapetumia jina lake kwenye Facebook na kusema kuwa hana akaunti yoyote katika mtandao huo mkubwa unaomilikiwa na Meta.
Rayvanny alipakia picha ya tangazo hilo na kusema kuwa hana akaunti yoyote kwenye Facebook.
“Sina akaunti yoyote kwenye Facebook,” Rayvanny alisema.
Ziara ya haraka kwenye ukurasa huo, tuligundua kwamba ulikuwa na kila kitu kilichokuwa kwenye ukurasa wa Rayvanny wa Instagram na hakukuwa na utofauti wowote wa kuonesha kuwa akaunti hiyo ni feki.
Kuanzia kwa picha za matukio mbalimbali ambayo msanii huyo amekuwa akifanya ndani ya nje ya Afrika zilikuwa zimepakiwa siku na muda sawa na zile ambazo amepakia kwenye Instagram yake, jambo ambalo lilitia ukakasi Zaidi kuhusu yeye kuikana akaunti hiyo – ambayo tayari hadi imedhibitishwa na Facebook kwa kupewa alama ya buluu kama halali kwa msanii husika.
Lakini wengine walihisi akaunti hiyo huenda ilikuwa yake kwa muda Fulani kabla ya kudukuliwa na mtu ambaye anamfuatilia kwa karibu kuona maisha yake Instagram na kupakia sawia Facebook ili kuwaaminisha mashabiki wake kuwa ni yeye.