Rostam Asalimu Amri kwa Chama cha Majaji Tanzania "Niliteleza Ulimi"
Mfanyabiashara, Rostam Aziz amekiangukia Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), akiomba radhi kutokana na kauli aliyoitoa dhidi ya Mahakama nchini.
Rostam ameomba radhi saa chache baada ya JMAT kutoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari, kikimtaka mfanyabiashara huyo athibitishe tuhuma alizotoa dhidi ya Mahakama au aombe radhi hadharani.
Rostam, Juni 26, mwaka huu mbele ya waandishi wa habari alisema, "Hakuna mwekezaji atawekeza kwenye nchi ambayo kesi ikipelekwa hapo Kisutu kiongozi yoyote anaweza kupiga simu akaielekeza mahakama nini cha kufanya.”
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Rostam alizungumzia faida za uwekezaji wa sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari, akirejea mkataba wa ushirikiano uliosainiwa na Serikali ya Tanzania na Dubai kuhusu uwekezaji na uendelezaji wa bandari nchini.
Hata hivyo, sakata hilo limeibua hisia tofauti za wananchi, wengine wakikosoa kutokana na kile wanachoeleza kuwa, baadhi ya vifungu vya mkataba huo vina kasoro na hatari kwa masilahi ya nchi.
JMAT ilitangaza kusikitishwa na kauli hiyo ikisema, "Anapaswa athibitishe kauli yake akibainisha jina la Jaji na lini alipewa maagizo na Serikali kutoa maamuzi kinyume na taratibu zilizopo. Akishindwa kutoa uthibitisho, tunamtaka atumie jukwaa lile lile kuomba radhi kwa uzito ule ule.”
Baada ya taarifa hiyo, Rostam leo Jumanne, Julai 4, 2023 amezungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, akieleza alichokizungumza siyo kusudio lake ni kuteleza kwa ulimi. "Kwa sababu ya kutambua na kuheshimu dhima, hadhi na wajibu wa kikatiba wa Mahakama, ningependa kusema yafuatayo.
"Ningependa kuuhakikishia umma, kwamba wakati nikizungumzia uwekezaji halikuwa kusudio langu kuidharau Mahakama," amesema.
Alichokizungumza, amesema ameteleza ulimi na si kusudiolake.
"Niliteleza ulimi, maana kusudio langu lilikuwa ni kueleza kuhusu uwekezaji nchini na maana yangu ilikuwa ni kwamba, ili tupate uwekezaji nchini hatuna budi kuendana na taratibu," amesema.