Ripoti ya uchunguzi ya mwili wa mwanafunzi Sixtus Kimario (7), anayedaiwa kupigwa viboko na mwalimu wake inaonyesha kifo chake kilisababishwa na damu kuvujia kwenye ubongo.
Sixtus, aliyekuwa akisoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Samanga, kata ya Kirongo Samanga, wilayani Rombo, anadaiwa kuchapwa na mwalimu wake hadi kufariki dunia kwa kinachodaiwa alikuwa akipiga kelele darasani.
Julai 17, mwaka huu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alithibitisha tukio hilo, akisema baada ya tukio hilo, mwalimu anayetajwa kuwa James Urassa alitoroka na anaendelea kutafutwa.
Katika uchunguzi wa kitabibu uliofanywa juzi katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC, ndugu wa marehemu, Odilo Shayo alisema imebainika kifo chake kilitokana na kuumia sehemu ya ubongo wa nyuma hivyo damu kuvuja.
Shayo, aliyeshiriki mwanzo hadi mwisho wa uchunguzi huo, alisema daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa mtoto, aliwaeleza sehemu ya nyuma ya ubongo kuna mpasuko.
Ameiomba Serikali kuingilia kati na kumchukulia hatua kali mwalimu huyo. “Tunaamini Serikali kupitia vyombo vyake vitalifanyia kazi na haki itapatikana," amesema.
Julai 17, mwaka huu, babu wa mwanafunzi huyo, Patrick Kachomba alisema mtoto huyo alipoondoka nyumbani kwenda shule hakuwa na tatizo lolote hadi walipopatiwa taarifa kuwa amefariki dunia.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Charles Chavunike alipoulizwa kuhusu taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo alikiri na kuongeza kuwa tukio hilo lilitokea saa tatu asubuhi Julai 17, mwaka huu.
Amesema aliwaita wanafunzi wawili waliokuwepo darasani na alipowahoji kuhusu tukio hilo walimweleza mwalimu aliwachapa kutokana na kupiga kelele.