JEDAH, SAUDI ARABIA.MMESIKIA? Baada ya kufanya vibaya kwa msimu uliopita sasa mabosi wa Al Nassr wameamua kufanya kweli kuelekea msimu ujao ambapo mbali ya kummiliki Cristiano Ronaldo na kuwasajili baadhi ya mastaa, sasa imemchukua na staa wa kimataifa wa Senegal kutoka Bayern Munich, Sadio Mane ambaye hadi sasa kila kitu kipo sawa na yupo kwenye hatua za mwisho kumwaga wino.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ni kwamba Munich imekubali kumuuza fundi huyu kwa kiasi cha Pauni 34 milioni ikiwa ni baada ya mazungumzo ya kina kati ya benchi la ufundi na mchezaji mwenyewe ambaye alionyesha anahitaji kuondoka na kupata changamoto mpya sehemu nyingine kwani hakuwa na furaha tena kuendelea kusalia kwenye kikosi hicho.
Mbali ya kuuzwa kwa kiasi hicho, fundi huyu ambaye alijiunga na Munich akitokea Liverpool mwaka jana, ataenda kupokea mshahara sawa na pesa aliyonunuliwa Pauni 34 milioni kwa mwaka.
Kwa msimu uliopita Mane alicheza mechi 38 za michuano yote akiwa na mabingwa hawa wa Ujerumani, akafunga mabao 12 na kushinda taji la Bundesliga .
Al Nassr inaonekana haitanii hata kidogo baada ya kuambulia patupu ikikosa hata kikombe kimoja kwa msimu uliopita katika dirisha hili imefanikiwa kuwapata Marcelo Brozovic kutoka Inter Milan, Seko Fofana kutoka Lens na Alex Telles aliyetua akitiokea Manchester United.
Vilevile imemchukua Anderson Talisca na kipa wa zamani wa Arsenal David Ospina, huku malengo yakiwa ni kuchukua ubingwa baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa msimu uliopita ilipomaliza nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Al-Ittihad kwa tofauti ya alama tano.
Mane ambaye ana uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya mbili anaweza kuwa mshambuliaji wa kati, winga wa kushoto na kulia, usajili wake unaenda kuongeza mabao kwenye eneo la ushambuliaji la Al Nassr ambapo kwa msimu uliopita ni Ronaldo aliyekuwa kinara kwa kuwa na mabao 14 .
Baada ya kufanya vizuri kwenye akademi ya Generation Foot, Mane alianza maisha yake ya soka ya Ulaya kwenye viunga vya Metz kabla hajajiunga na Red Bull Salzburg mwaka 2012 na baada akatua Southampton mwaka 2014 kabla kuchukuliwa na Liverpool miaka miwili baadaye.
Kwenye maisha yake ya soka hadi sasa ameweka rekodi nyingi na kupata mafanikio makubwa kwani akiwa hapo ameshinda mataji ya Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa, FA Cup na Kombe la Ligi.
Maisha yake kwenye viunga vya Munich hayakuwa mazuri kwani akiwa hapo alishindwa kuwa sehemu ya kikosi cha Senegal kilichoshiriki michuano ya Kombe la Dunia kule Qatar mwaka jana baada ya kukumbuwa na majeraha, pia alisimamishwa baada kumpiga kiwiko staa mwenzake Leroy Sane wakati walipokuwa kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Manchester City.