Serikali kupitia Wizara ya Afya, imetoa ajira ya mkataba kwa Mariam Mwakabungu (25), mwanamke anayejitolea kukumbatia watoto njiti waliotupwa na kutelekezwa katika Hosptali ya rufaa ya mkoa Amana.
Ajira hiyo imekuja siku moja tangu Rais Samia Suluhu Hassan kutuma salamu za pongezi zilizoambatana na fedha taslimu Sh2 milioni.
Julai 16, gazeti na la Mwananchi pamoja na mitandao yake ya kijamii, lilichapisha habari kuhusu Mariam ambaye ameokoa maisha ya watoto njiti watatu hospitalini hapo, kwa kuwakumbatia kwa njia ya kangaruu baada ya kutelekezwa na mama zao.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamis Julai 20, 2023 Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameeleza utaratibu utakaotumika katika kumpa ajira hiyo.
"Tutampa ajira ya mkataba kwanza…tutamshauri ajiendeleze kielimu….Madaktari wanasema yule mama anajitoa na anapenda kufanya hiyo kazi ana moyo yaani ni kitu anapenda…itabidi aingizwe katika utaratibu huo ili aweze kupata sifa," amesema Waziri Ummy na kuongeza;
"Ana miaka 25 bado ana muda anaweza kusoma uuguzi ngazi ya astashahada akawa muuguzi wa watoto njiti,’” amesema Waziri Ummy na kuongeza;
“Tunaendelea kumpongeza na tutamshauri ajiendeleze kielimu ni jambo zuri na tumemuomba afanye hivyo."
Hata hivyo Waziri Ummy amesema ni jambo zuri alilofanya kwani wauguzi wa zamani walikuwa ni watu wanaopenda kazi ya uuguzi na wana upendo, walio wengi kwa sasa wanaingia katika kazi hiyo kutafuta tu ajira.
Alipoulizwa iwapo Serikali inafikiria kutoa ajira hizo kwa watu wengi zaidi ili kuokoa maisha ya watoto njiti amesema wanahitaji wenye moyo wa kujitolea kwanza ndipo wafikirie kuwaajiri.
"Kama tutapata watu kama hao kwakweli tutakua tunawaajiri kwa mkataba, nikitoa wito watafurika wengi kwa sababu watu hawana ajira," amesema Waziri Ummy.
Mariam ambaye ni mke na mama wa watoto wawili, alianza kutoa msaada huo baada ya kumtembelea rafiki yake aliyejifungua mtoto njiti na kumuona mtoto ambaye aliishi kwa muda wa miezi minne bila kuongezeka uzito.
Anasimulia kuwa alipomuona njiti huyo wito ukamjia na kukumbuka kuwa yeye ni yatima ambaye hakupata bahati kulelewa na wazazi hivyo akaona hilo ni jukumu lake.
"Sijalelewa na wazazi wawili walishafariki kwahiyo nikajitoa kusaidia. Mtoto wa kwanza ambaye nilimsaidia nilimkuta ameishi kwenye mashine kwa muda mrefu na haongezeki uzito kwahiyo hakui, niliingia imani nikaona nimtunze angalau akue ajitegemee.
"Manesi walimweka kifuani kwangu nikaishi naye ndani ya wiki moja akaongezeka uzito kutoka gramu alizokuwa nazo akafikisha kilo moja na kuongezeka kilo ya pili," anasema Mariam ambaye ni mfanyabiashara ndogo ndogo.
Anasema alipokamilisha azma yake, kabla ya kuondoka kina mama wawili waliojifungua njiti, walitelekeza watoto na kukimbia hivyo ikamlazimu nao awatunze.