Simba tayari imeanza kutambulisha nyota wapya wa kikosi kipya cha msimu ujao ikiwa imepania kufanya vizuri zaidi na sasa imeita vifaa vyote vya zamani na wapya sambamba na benchi la ufundi lote Dar es Salaam ili kupewa darasa maalumu kabla ya kupaa kwenda Uturuki itakapoweta kambi.
Kambi hiyo ya maandalizi ya msimu mpya (Pre Season) inatarajiwa kuanza wiki ijayo na awali ilikuwa baadhi ya wachezaji waende moja kwa moja Uturuki, bila ya kuja Bongo, akiwemo kipa Mbrazili Caique Luiz Santos aliyepanga kuambatana na kocha mkuu Roberto Oliveira 'Robertinho' lakini viongozi wamebadili gia angani na kuwataka wote watue Dar mapema kabla ya Julai 10, ili wapewe darasa kisha kwenda Uturuki.
Simba inataka kuwakusanya wachezaji na makocha wote itakaowatumia kwa msimu ujao, iwatambulishe na kuwaonyesha ukubwa wa timu hiyo kisha kuwapa malengo, mikakati na vitu wanavyotakiwa kufanyia kazi katika msimu ujao.
Miongoni mwa nyota wapya ambao Simba ina uhakika wa kuwa nao kwa maandalizi ya msimu ujao kama mambo yasipobadilika ni kipa Caique, beki wa kati Che Malone kutoka CotonSports ya kwao Cameroon, mshambuliaji Mcameroon Andre Onana aliyeibuka mchezaji bora na mfungaji bora wa ligi ya Rwanda msimu uliopita akicheka na nyavu mara 17 moja na winga Kramo Aubin kutoka Asec Mimosac ya Ivory Coast ambaye ilielezwa alikuwa hatua ya mwisho kusaini Msimbazi.
Banda, Onyango bado
Katika hatua nyingine Simba bado haijamalizana na wachezaji wawili walioomba kuondoka kikosini hapo, Winga Mmalawi, Peter Banda na beki Mkenya Joash Onyango.
Simba ilipanga mwanzo kumtoa Banda kwa mkopo katika moja ya timu za ligi kuu lakini inaelezwa machachari huyo aligoma na kutaka alipwe mkwanja asepe zake jambo ambalo hadi sasa Simba inalitafutia ufafanuzi.
Kwa upande wa Onyango aliomba kuondoka Simba kutokana na kutokuwa na furaha ndani ya kikosi hicho pia kutotimiziwa baadhi ya matakwa yake lakini niu kama bado mabosi wa timu hiyo wanasita kumuachia wakihofia kukosa mbadala wake na kama watamuacha basi huenda akatua Singida Fountain Gate.
Hata hivyo, kama Simba itakamilisha usajili wa Caique, Onana, Malone, Aubin na Fabrice Ngoma basi itahitaji kupunguza wachezaji wawili wa kigeni ili wabaki 12 kama wanaotakiwa.
Kwa sasa Simba licha ya kutembeza 'Thank You' kwa baadhi ya wachezaji wake wa kigeni, imebaki na mapro tisa ambao ni Jean Baleke, Saidi Ntibazonkiza, Clatous Chama, Banda, Pape Sakho, Moses Phiri, Onyango, Sadio Kanoute, na Henock Inonga jambo linaloendelea kuwaumiza vichwa viongozi wamtoe nani licha ya kwamba Banda na Onyango wameonesha nia ya kuondoka.
"Usajili unaendelea na tutashusha majembe ya maana lakini kuhusu hilo la Banda na Onyango bado hatujafika mwisho naomba tuachane nalo likitimia nitakujuza," alisema kiongozi wa Simba.
Simba hadi sasa imeachana na wachezaji Beno Kakolanya, Gadiel Michael, Mohamed Ouattara, Ismael Sawadogo, Victor Akpan, Nelson Okwa, Jonas Mkude, Erasto Nyoni na Augustine Okrah.