Simulizi kijana aliyeoa wake watatu kwa mpigo Katavi



Katavi. “Mpaka nafikia hatima ya kuoa wanawake watatu si tamaa. Nilifikiria sana, hapo mwanzo nikiwa na umri wa miaka 18 nilioa mwanamke mmoja alinisumbua sana.”


Hiyo ni kauli ya Athuman Yegayega (25), mkazi wa Shanwe, Manispaa ya Mpanda, Mkoa wa Katavi ambaye Jumamosi iliyopita alifunga ndoa na wanawake watatu siku moja.


Ndoa hiyo imeibua mijadala ndani na nje ya mkoa huo kutokana na uamuzi wa Yegayega kufungishwa ndoa hiyo na Sheikh
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mashaka Kakulukulu huku akidokeza siku zijazo ataongeza mke mwingine wafikie wanne.


Sheikh Kakulukulu alifungisha ndoa hizo baina ya Yegayega na wake zake Fatma Raphael (30), Aisha Pius (20) na Mariam Manota (21) na ndoa zilipishana kwa dakika 10 huku akisema hilo ni jambo la kawaida.


"Hili ni funzo kwetu kwamba suala hili la uke wenza si la ajabu ni la kawaida, manabii na mitume walifanya hivyo, utaratibu niliotumia ni kumfungisha ndoa na mke mmoja kila baada ya dakika 10," alisema Sheikh Kakulukulu alipozungumza na gazeti hili


Alisema uamuzi wa kijana huyo kufunga na wanawake watatu lina faida, linapunguza watoto wa mitaani kwa sababu watu wakiwa wanandoa watapata kizazi ambacho watakitunza kama baba na mama.


“Manufaa mengine ni kupunguza idadi ya wanawake wasiokuwa na waume mitaani, hali inayojionyesha wazi wanawake ni wengi duniani,” alisema.


Kiongozi huyo wa dini, alisema hilo si tukio la kwanza mkoani hapo, kwani miaka miwili iliyopita alifungisha ndoa ya mwanaume na wanawake wawili kwa wakati mmoja.


“Kwa upande wetu wa dini ya Kiislamu, kama Mungu alivyosema sura ya nne aya ya tatu, oeni wanawake mnaowapenda wawe wawili, watatu au wanne,” alisema.


Baada ya kumaliza kuzungumza na kiongozi huyo wa dini, gazeti hili lilizungumza na wanandoa hao wanaoishi kwa sasa kwa kaka yake, Kawajense alipowafikishia baada ya kufunga ndoa hizo.



Alisema amechukua uamuzi huo baada ya miaka ya nyuma akiwa na umri wa miaka 18 kuoa mwanamke ambaye alimsumbua.


“Sikufunga naye ndoa, nilimchukua kwa makubaliano yangu, yeye na wazazi wake huko kijiji cha Kasekese. Migogoro ilikuwa mingi na baadaye tuliamua kuachana. Sababu kubwa ya kuondoka ni uchumi wangu ulikuwa mdogo,” alisema.


Alisema wakati akiishi na mwanamke huyo hawakubahatika kupata watoto, hivyo alipoondoka alikaa muda mrefu bila kuoa, huku akiendelea na shughuli zake za kilimo na biashara.


Huku akionekana mwenye tabasamu, Yegayega alisema baada ya kukaa muda mrefu bila kuoa, alifikiria kuoa, lakini si mwanamke mmoja ili kuepuka yaliyomkuta kwamba akiachwa atabaki mpweke.


Alisema alianza kumuoa Fatma, mkazi wa Kigoma ambaye alikuwa akiishi naye na kubahatika kupata watoto wawili.


“Nilikuwa nimjengea nyumba Shanwe na nilimwambia nitaoa wanawake wengine watatu wafike wanne na nifunga nao ndoa siku moja.


“Alikubali, nikatafuta mwanamke wa pili, Aisha Pius, mkazi wa Subawanga niliyezaa naye mtoto mmoja wakati wa uhusiano wa kimapenzi siku za nyuma,” alisema.


Alisema alimweleza Aisha kwamba ana mke, lakini anahitaji kuongeza wake wengine watatu.


“Mwanzo alikuwa haelewi, lakini baadaye alikubali. Nikampata Mariam Manota, mkazi wa Tabora ambaye ni fundi cherehani, wote wakaridhia,” alieleza.


Kutokana na gharama kuwa kubwa za mahitaji ya ufungaji ndoa na kuwaandalia nyumba za kupanga wanawake wawili, alishindwa kutafuta mke wa nne na kuahidi atafanya hivi siku zijazo.


“Baada ya kumaliza majukumu haya, nitaongeza mke wa wanne yupo tayari nilishamuandaa. Nawahudumia vizuri tu wake zangu, watakula milo mitatu kwa siku.


“Natarajia kupata watoto 40, kila mmoja azae watoto 10. Kwa sasa nina wanne, mmoja nilikuwa naye. Baba yangu alioa wanawake watatu, tumezaliwa watoto wengi, hata idadi siijui,” alisema.


Alisema atahakikisha waatoto wake wanasoma vizuri na kwamba mpaka sasa walio na umri wa kwenda shule wanasoma.


“Nawahudumia kwakila kitu, napenda kuwa na familia kubwa,” alisema.


Hataki zamu kwa wake


Pamoja na hayo, alisema anatoa huduma kwa uwiano, lakini si kwa kupangiwa na mwanamke hususani zamu za kulala.


“Nimeshawaeleza kila mmoja atakuwa na familia yake, hivyo siku nikijisikia kwenda kwa mkubwa au mdogo hakuna wa kuuliza.


“Nina majukumu mengi, kwa hiyo naweza kuchagua mwenyewe sehemu ya kulala si kupangiwa. Nimeshawaeleza na wamenielewa,” alisema.


Pi, alisema matarajio yake ni kuwaendeleza wake zake kutokana na vipaji vyao.


"Bi Fatma ni mfanyabiashara wa mazao ataendelea na biashara yake, huyu Aisha atakuwa mama wa nyumbani atanihudumia kila kitu. Mariam ataendelea na ushonaji nguo, jioni atauza vinywaji kwenye biashara yangu," alisema.


Kuhusu elimu, alisema alisoma moaka darasa la nne, hakuweza kuendelea na masomo baada ya kuamua kujishughulisha na kilimo pamoja na biashara.


“Nilikuwa sipendi shule, nilianza kulima nikiwa mdogo huko Kibo, Tanganyika. Nalima mpunga na mahindi mwaka huu, nimevuna gunia 100 za mahindi,” alisema.








…tunapendana, hatuna wivu


Mke mkubwa, Fatma alisema hadi mumewe aamue kufunga ndoa na wake wengine alishirikishwa na akaridhia, hivyo yuko tayari kwa lolote.


“Sina wivu, badala ya kuendelea na michepuko bora aoe wake wengi atulie. Anatuhudumia vizuri, siku ya ndoa tulilala kitanda kimoja wote tunapiga stori,” alisema huku akitabasamu


“Anatambua majukumu yake vizuri, matumizi anatoa. Mimi nafanyabiashara ya mazao, nachangia mahitaji mengine kwa hela yangu,” alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad